Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma, ameishauri Serikali kupitia upya masharti mapya yanayowataka madereva walioko kazini kufanyiwa mafunzo na mitihani upya ili kuhuisha leseni zao, akisema utaratibu huo unaweza kuhatarisha ajira na maisha ya maelfu ya wananchi wanaotegemea udereva kama chanzo cha kipato.

Akichangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali bungeni, Musukuma amesema kuna madereva wengi nchini ambao wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 bila kusababisha ajali kubwa, hivyo hawapaswi kulazimishwa kurudi darasani na kufanya mitihani inayoweza kuwaondoa kazini.

Amesema utekelezaji wa masharti hayo mapya unaweza kuwaongezea mzigo mkubwa madereva wenye kipato cha chini, ambao tayari wanakabiliwa na changamoto za kifamilia na maisha ya kila siku yanayotegemea mshahara wao wa kila mwezi.

Mbunge huyo pia ametumia nafasi hiyo kuikosoa Serikali kuhusu baadhi ya miradi ya maendeleo, hususan ujenzi wa masoko na stendi za kisasa, akidai kuwa baadhi ya miradi hiyo haitimizi mahitaji halisi ya wananchi katika maeneo husika.

Katika hoja nyingine, Musukuma amepinga matumizi makubwa ya fedha za umma katika maonesho, mikutano na warsha za watumishi wa umma, akisema shughuli hizo zinagharimu Serikali fedha nyingi kupitia safari, malazi na posho, fedha ambazo angependa zielekezwe zaidi kwenye huduma za maendeleo.

Badala yake, ameshauri Serikali kuimarisha matumizi ya teknolojia za mawasiliano, ikiwemo mikutano ya mtandaoni, ili kupunguza gharama zisizo za lazima na kuongeza ufanisi katika utendaji wa shughuli za serikali.