Takriban watu 28 wamefariki dunia kufuatia moto mkubwa ulioteketeza kiwanda cha kutengeneza viatu katika mji wa Jinjiang, kusini mashariki mwa China, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali, Xinhua.
Picha za video zilizochapishwa na Xinhua zilionesha moshi mzito mweusi ukifuka kutoka kwenye jengo la kiwanda, huku baadhi ya watu wakionekana wamenaswa juu ya paa wakisubiri kuokolewa.
Rais wa China, Xi Jinping, alisema moto huo umesababisha "vifo vingi", na kusisitiza kuwa yeyote atakayebainika kuwajibika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mji wa Jinjiang, ulioko katika jimbo la Fujian, unajulikana kama "mji mkuu wa viatu" wa China kutokana na kuzalisha takribani asilimia 20 ya viatu vya michezo vinavyotengenezwa duniani.
Moto huo ulizuka katika kiwanda cha Huiteng Footwear majira ya saa sita mchana kwa saa za eneo hilo siku ya Alhamisi.
Mamia ya waokoaji walipelekwa eneo la tukio, huku zaidi ya watu 200 wakihamishwa kutoka kiwandani kwa usalama, kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya CCTV.
Bado haijafahamika ni watu wangapi wamejeruhiwa.
Mamlaka zilisema zaidi ya wafanyakazi 500 wa zimamoto na uokoaji walitumwa kuzima moto huo na kuwaokoa watu waliokuwa wamenaswa ndani ya kiwanda.
0 Comments