
Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, amemshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutumia hekima na busara zilizomwongoza kutangaza sera ya 4Rs ili kumaliza changamoto zinazomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Julai 13, 2026, Prof. Tibaijuka amesema anaamini kesi inayomkabili Lissu haikamiliki na hivyo amependekeza hatua ya kumuachia huru.
“Dkt. Samia Suluhu, Rais, naendelea kushauri kwa dhati Tundu Lissu aachiwe huru kwani kesi haikamiliki. Hekima na busara iliyokufanya kutangaza sera ya 4Rs mara ulipoingia madarakani ikuongoze tena katika jambo hili,” aliandika.
Aidha, Prof. Tibaijuka amesema taarifa zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu hali hiyo zimeibua hisia mbalimbali kwa wananchi, hususan vijana, huku akieleza kuwa zinaweza kuathiri taswira ya Tanzania kimataifa.

“Simulizi hizi za kutisha za Vyombo vya Habari vya Kimataifa zinaibua hisia kali hasa kwa Vijana. Hata Wazee tumekumbushwa kadhia ya Operation Sogeza iliyounda Vijiji vya Ujamaa 1974–1976. Taarifa hizi zinaathiri kikubwa taswira ya Taifa letu na maslahi yake,” alisema.
Katika ujumbe wake, Prof. Tibaijuka amesisitiza umuhimu wa kutafuta muafaka kupitia uwajibikaji na maridhiano, huku akiwataka Watanzania kuwa na hofu ya Mungu na kuliombea Taifa.
Amehusisha pia kauli yake na tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Tundu Lissu mwaka 2017, akisema ni jambo linalopaswa kutafakariwa katika muktadha wa imani na hatima ya maisha.

0 Comments