Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba yeyote atakayevunja atashughulikiwa.

Ameyasema hayo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA), jijini Arusha.

Rais Samia amesema Tanzania iko vizuri kwenye masuala ya haki za binadamu na uzuri ni kwamba hakuna aliye juu ya sheria, anayevunja sheria anashughulikiwa.

''Tanzania tuko vizuri, waendelee kusema hakuna haki,tunavunja haki, lakini hakuna aliye juu ya sheria''.

"Tunashuhudia mataifa yakihujumiana, tunashuhudia vijana kulaghaiwa na kumezeshwa sumu dhidi ya mataifa yao na kushawishiwa kuhujumu chumi zao zilizojengwa kwa nguvu kubwa".

"Vilevile kuna wimbi la kuwaaminisha vijana kwamba serikali zao hasa za Afrika, hazifuati au zinakiuka haki za binaadamu". Alisema Rais Samia.

"Sasa hapa ninataka tukumbushe tu ulimwengu lakini na watu wetu wajue kwamba kwa upande wa Tanzania, sisi ni wafuasi wazuri sana wa haki za binadamu.'' Mtakumbuka kwamba sisi Tanzania tuliweka kwa mara ya kwanza kwenye Katiba yetu, mtiririko wa haki za binadamu tulipobadili sheria mwaka 1984 na tukatanua wigo wa haki hizo.

Rais Samia amewataka mawakili kutekeleza kwa weledi majukumu yao na kutoa majawabu kwa changamoto zinazojitokeza.

"Niseme nyinyi ni walinzi muhimu wenye ujuzi wa kisheria za ndani na za kimataifa, nimesema hali ilivyo duniani sasa hivi, lazima tuwe na weledi wa matamko, itifaki na mambo mengine ya kimataifa yanayotoka huko, kuyaangalia kwa haraka, kuyatafsiri katika hali yetu na kutoa majawabu kwa haraka ili kuuhami uhuru wetu". Alisema.