Picha ya Kiiza Besigye

Mke wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza BesigyeWinnie Byanyima amelaani hatua ya kuendelea kusikilizwa kwa kesi ya Besigye kwa siku ya pili, huku mwanasiasa huyo akiwa amelazwa gerezani.

Besigye, mwenye umri wa miaka 70, amekuwa kizuizini, akikabiliwa na mashtaka ya uhaini kutokana na madai ya kupanga njama ya kutaka kumpindua Rais wa muda mrefu, Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka wa 1986.

Winnie Byanyima, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS, ameshtumu vikali kuendelea kwa kesi hiyo wakati Besigye hawezi kufika mahakamani kutokana na hali yake ya kiafya.

“Hii si kesi, ni utani, kwa sababu Kizza Besigye hajakataa kufika mahakamani amelazwa kitandani, ni mgonjwa sana, hawezi kuzungumza,” Byanyima aliiambia shirika la habari la AFP.

Besigye alitekwa nyara nchini Kenya mwaka 2024 na baadaye kusafirishwa hadi nchini Uganda, ambako alifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi kabla kesi yake kuhamishiwa katika mahakama ya kiraia.

Mwanasiasa huyo awali alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) baada ya kuanguka akiwa mahakamani, lakini alirejeshwa gerezani mapema mwezi huu licha ya ushauri wa madaktari kuwa hali yake ya afya si nzuri.

Mapema mwezi huu, Byanyima aliiomba serikali ya Uganda imwachilie Besigye kwa dhamana ili aweze kupata matibabu.