Dozi elfu 70,000 za chanjo ya Ebola zitapelekwa nchini DRC, ili kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo.
Kundi la Kimataifa la Kuratibu Ugavi wa Chanjo limesema kuwa shehena hiyo inajumuisha dozi elfu 50,000 kwa ajili ya wahudumu wa afya walioko katika mstari wa mbele katika kukabiliana na mlipuko huo ambao maambukizi yake yanazidi kuongezeka kila siku.
Dozi hizo 70,000 ni za chanjo ya Ervebo, iliyotengenezwa kupambana na aina ya virusi vya Ebola ya Zaire ambayo ndiyo ya kawaida zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuwa chanjo hiyo imeonyesha ufanisi fulani katika majaribio dhidi ya aina adimu ya Ebola ya Bundibugyo, ambayo inaenea nchini DRC kwa sasa
Kati ya dozi hizo,elfu 20,000 zinazopelekwa nchini humo zimetengwa kwa ajili ya majaribio ya kitabibu, huku zilizosalia zikiwa kwa ajili ya wahudumu wa afya walio katika mstari wa mbele.
Chanjo mbili tofauti zilizotengenezwa mahususi dhidi ya aina hiyo ya virusi pia zinaanza kufanyiwa majaribio kwa binadamu kwa mara ya kwanza.
Hadi kufikia sasa, imethibitishwa kuwa watu 2,378 wamefariki dunia kutokana na Ebola huko DRC, huku kukiwa na visa 5,021 vilivyothibitishwa.
0 Comments