Serikali ya Tanzania imewapa wazalishaji wa saruji muda wa siku nane kuongeza usambazaji na kushusha bei, baada ya mfuko wa saruji wa kilo 50 kufikia hadi shilingi 26,000 pesa za Tanzania sawa na dola 9.8 katika baadhi ya maeneo.
Wizara ya Viwanda na Biashara iliitisha kikao cha dharura na wazalishaji tarehe 18 Agosti, na kuwapa hadi Agosti 28 kuchukua hatua za kukabiliana na upungufu wa saruji na kupunguza bei.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Rajabu Salum, amesema serikali itafuatilia kwa karibu bei na upatikanaji wa saruji kabla ya kuamua iwapo hatua zaidi zitahitajika.
Wazalishaji wamehusisha upungufu wa bidhaa hiyo na hitilafu katika baadhi ya mitambo mikubwa ya uzalishaji wa klinka, ikiwemo kiwanda cha Maweni mkoani Tanga na Dangote. Wasambazaji, kwa upande wao, wametaja kupanda kwa gharama za mafuta na usafirishaji.
Hata hivyo, tofauti kati ya bei ya saruji kutoka kiwandani na ile ya rejareja imeibua maswali kuhusu ongezeko la bei katika mnyororo wa usambazaji.
Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kuwa saruji ilikuwa ikiuzwa kwa wastani wa shilingi 321,251 pesa za Tanzania sawa na dola 121.47 kwa tani kabla ya kodi ya ongezeko la thamani, sawa na takriban shilingi 16,063 kwa mfuko wa kilo 50.
Baraza la Taifa la Ujenzi linasema ongezeko la mahitaji ya ujenzi, gharama za usafirishaji na kuvurugika kwa usambazaji ni miongoni mwa sababu zinazochangia kupanda kwa bei.
Hatua ya serikali inakuja wakati bei ya saruji ikiwa na athari kwa gharama za ujenzi, huku watumiaji na wafanyabiashara wakisubiri kuona iwapo agizo hilo litashusha bei katika siku zijazo.
0 Comments