Watalii sita na rubani wamefariki dunia baada ya helikopta waliokuwa wakisafiria kuanguka katika Mlima Ololokwe, Kaunti ya Samburu, kaskazini mwa Kenya, maafisa wa uchunguzi wa ajali za ndege wameiambia BBC.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya, KCAA, imesema ajali hiyo ilitokea takriban saa 9:13 asubuhi kwa saa za Kenya.
Kwa mujibu wa KCAA, helikopta hiyo ilikuwa kwenye safari ya kitalii kutoka hifadhi ya wanyamapori ya Loisaba kuelekea Ewaso Nyiro, mto unaopita katika maeneo kadhaa ya hifadhi za taifa.
Picha iliyosambaa mtandaoni inaonyesha moshi ukitoka katika eneo la ajali kwenye Mlima Ololokwe.
Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limeiambia BBC kuwa eneo la ajali bado halijafikika, lakini ndege zisizo na rubani zinatumika kutathmini hali katika eneo hilo.
KCAA imesema helikopta hiyo ilikuwa aina ya Eurocopter EC130 B4 na kwamba inaongoza uratibu wa shughuli zinazohusiana na ajali hiyo.
Wizara ya Uchukuzi pamoja na Idara ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege zitaongoza uchunguzi wa “mazingira yaliyopelekea ajali hiyo”, KCAA imeongeza.
Kaunti ya Samburu ni miongoni mwa maeneo maarufu ya utalii nchini Kenya, ikiwa na hifadhi kadhaa binafsi za wanyamapori na inayojulikana kwa mandhari yake ya kuvutia.
Ajali za helikopta zimewahi kutokea mara kadhaa nchini Kenya.
Mwezi Februari, watu sita, akiwemo mbunge mmoja, walifariki dunia baada ya helikopta kuanguka katika Kaunti ya Nandi, eneo la Bonde la Ufa.
Mwaka 2024, Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla, alifariki baada ya helikopta ya kijeshi iliyokuwa imewabeba watu 11 kuanguka magharibi mwa nchi. Watu wawili pekee walinusurika.
Mwezi Juni 2021, angalau wanajeshi 10 walifariki baada ya helikopta yao kuanguka wakati ikijaribu kutua karibu na Nairobi.
0 Comments