Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia dereva wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Dodoma, Sath John Masawa (31), kwa tuhuma za kumtishia dereva wa basi la SATCO kwa kutumia kitu kinachodhaniwa kuwa bastola, kufuatia tukio la mgongano wa magari lililodaiwa kutokea jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, tukio hilo lilihusisha basi la SATCO aina ya Yutong, lenye namba za usajili T 308 EME, lililokuwa likiendeshwa na Said Fadhili (54), ambaye alidaiwa kukwanguliwa na gari aina ya Land Cruiser LX 70 Series linalomilikiwa na TARURA, wakati akitoka kuweka mafuta katika kituo cha TotalEnergies.

Baada ya tukio hilo, inadaiwa kuwa dereva wa gari hilo la TARURA, Sath John, alimtishia Said kwa kutumia kitu kilichodhaniwa kuwa bastola, hali iliyosababisha tukio hilo kuripotiwa katika Jeshi la Polisi.

Polisi walifika eneo la tukio na kumkamata Sath John. Baada ya kumfanyia upekuzi, ilibainika kuwa kitu alichokuwa amevaa kiunoni hakikuwa bastola halisi, bali ni toyi iliyotengenezwa kwa kufanana na bastola.

Katika uchunguzi wa awali, Jeshi la Polisi pia lilibaini kuwa gari la TARURA lililohusika katika tukio hilo, ambalo namba zake halali ni STM 5806, lilikuwa likitumia namba za usajili T 881 ENZ wakati wa tukio.

Kwa mujibu wa Polisi, namba hiyo inadaiwa kuwa ya gari jingine linalomilikiwa na mtu mwingine.

Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia Sath John kwa ajili ya mahojiano na kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewataka madereva kuacha kutumia namba za usajili zisizo halali kwenye magari, likieleza kuwa matumizi ya namba hizo yanaweza kuficha utambulisho halisi wa gari na ni kinyume cha sheria.