Na Oscar Assenga, TANGA
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa hati fungani wenye thamani ya Sh bilioni 53.12 kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha unakamilika ifikapo Novemba 30, mwaka huu, akisisitiza kuwa hakuna muda wa nyongeza utakaotolewa.
Aweso ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ikiwamo tanki kubwa la maji lililopo Mowe jijini Tanga, ambapo alisema serikali haitakuwa tayari kusikia visingizio kutokana na fedha za utekelezaji wa mradi huo kuwepo.
Alisema hadi sasa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 70 ya utekelezaji, hivyo mkandarasi anatakiwa kuongeza kasi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika na huduma hiyo kwa wakati uliopangwa.

“Nimekuja leo kukagua huu mradi nikiwa na Katibu Mkuu. Mradi huu sasa umefikia asilimia 75. Maelekezo ambayo nawaambia Tanga Uwasa na mkandarasi ni kwamba hatutakuwa na muda wa nyongeza.
“Utendaji wa mradi huu unatakiwa kubadilika kuanzia sasa. Mradi huu una fedha, hakuna kisingizio. Ni suala la mkandarasi kuongeza watu kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati,” alisema Aweso.
Aliongeza: “Utendaji ubadilike. Mkandarasi anatakiwa kufanya kazi usiku na mchana. Tunataka mwisho wa mwezi huu wa 10 tukija kuona maendeleo yake, yatupatie picha kwamba ifikapo Novemba 30, 2026, mradi utakuwa umekamilika.
“Hatuna kisingizio kwa sababu fedha zipo, na fedha hizi ni zile ambazo wananchi wameweza kujitolea kuchangia taasisi hii ya Tanga Uwasa.”

Aweso alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya mfano katika Wizara ya Maji inayotekelezwa kwa kutumia hati fungani kama chanzo mbadala cha fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma ya maji.
Alisema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na chanzo cha uhakika cha maji kitakachosaidia wananchi kupata huduma hata pale linapotokea tatizo la kiufundi au kukatika kwa umeme.
Kwa mujibu wa Aweso, hatua hiyo pia inaendana na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka taasisi za umma kuwa na vyanzo mbadala vya fedha ili kuongeza uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, alisema wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) katika kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba.
Alisema timu ya wizara itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Aweso, akisisitiza kuwa ifikapo Novemba 30, 2026, miundombinu yote inayohusika na mradi inapaswa kuwa imekamilika na wananchi kuanza kupata huduma.
TANGA UWASA
Mkurugenzi wa Tanga Uwasa, Geoffrey Hilly, alisema mradi huo unaendelea vizuri na kwa sasa umefikia wastani wa asilimia 72 kwa ujumla, ikiwamo kazi zinazotekelezwa na wakandarasi katika maeneo mbalimbali kuanzia chanzo hadi usambazaji wa mabomba mitaani.
Alisema mradi huo unalenga kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Tanga pamoja na Wilaya za Muheza na Mkinga, huku Mkinga ikiwa miongoni mwa maeneo yatakayonufaika zaidi na maji yanayozalishwa katika mtambo wa Mowe.
Kwa mujibu wa Hilly, mradi huo unahusisha upanuzi wa mtambo wa uzalishaji maji kutoka uwezo wa kuzalisha lita milioni 45 hadi lita milioni 60 kwa siku.
Alisema pia unahusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita milioni 35, litakalosaidia kuhakikisha maji yanapatikana hata katika vipindi vya changamoto za kiufundi.
Alisema tanki hilo lina uwezo wa kuhifadhi maji ya kutosha kwa matumizi ya takribani saa 18, hatua inayotarajiwa kusaidia wananchi kupata huduma ya maji kwa uhakika zaidi kwa saa 24.
MKANDARASI
Meneja wa mradi huo kutoka kampuni ya China Railway Seventh Group, Dai Bin, aliahidi kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha utekelezaji unakwenda kwa kasi ili kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliowekwa.
Dai alisema kampuni hiyo imepokea maelekezo ya Waziri Aweso na kwamba itaongeza muda wa kazi kwa kufanya shughuli za ujenzi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

0 Comments