
DODOMA; TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza Novemba 4, 2026 kuwa siku ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Mkoa wa Dodoma, pamoja na uchaguzi wa madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Ramadhani Kailima, uchaguzi huo unafanyika kufuatia kuwepo kwa nafasi wazi za uongozi katika maeneo hayo ya uchaguzi.
Taarifa hiyo imesema Tume ilipokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma.
Nafasi hiyo imejitokeza baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Deogratius John Ndejembi, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uteuzi huo ulifanyika Agosti 26, 2026 na kuthibitishwa na Bunge Agosti 28, mwaka huu.
Aidha, Kailima amesema Tume, kwa kuzingatia kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343, ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuhusu nafasi wazi za Madiwani 11 Tanzania Bara.
Amesema nafasi hizo zimetokana na vifo vya Madiwani wanane vilivyotokea kwa nyakati tofauti na Madiwani watatu kujiuzulu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, fomu za uteuzi kwa wagombea wa Ubunge Chamwino na Udiwani katika kata hizo zitatolewa kuanzia Oktoba 7 hadi 13, 2026, huku uteuzi wa wagombea ukifanyika Oktoba 13, mwaka huu.
Baada ya uteuzi, kampeni za uchaguzi huo zitaanza Oktoba 14 na kuendelea hadi Novemba 3, 2026, siku moja kabla ya uchaguzi.
Kailima amezitaja kata 11 zitakazofanya uchaguzi wa Madiwani kuwa ni Nonde katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Lugenge katika Halmashauri ya Mji Njombe, Bargish katika Halmashauri ya Mji Mbulu, Makole katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Mwera katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Oldonyosambu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Kata nyingine ni Igalula katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Shelui katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mvumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Nyarero katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.
Tume imevikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi chote cha utekelezaji wa ratiba hiyo.
0 Comments