Mahakama Kuu ya Kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeanza kusikiliza kesi dhidi ya makamanda wawili waandamizi wa jeshi wanaotuhumiwa kwa uoga na ukiukaji wa maadili ya kijeshi, makosa yanayodaiwa kuchangia mji wa Bukavu kuangukia mikononi mwa waasi wa M23 mwezi Februari 2025.
Kesi hiyo ilianza mjini Kinshasa, ambapo Meja Jenerali Yav Avul Robert, aliyekuwa kamanda wa operesheni za kijeshi Kivu Kusini, na Brigedia Jenerali Ehonza André Uketi, aliyekuwa mkuu wa operesheni katika jimbo hilo, walifikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yao.
Waendesha mashtaka wanadai maafisa hao walionyesha uoga vitani na kusababisha kudhoofika kwa maadili ya wanajeshi, hali iliyochangia kupotea kwa udhibiti wa Bukavu. Pia wanatuhumiwa kuongoza operesheni za kijeshi bila kuwa na uwezo wa kutosha wa kushambulia.
Kusikilizwa kwa kesi hiyo kulisitishwa muda mfupi baada ya mashtaka kusomwa, kufuatia ombi la mawakili wa utetezi la kupewa muda zaidi wa kuandaa majibu yao. Makosa yanayowakabili adhabu yake ni kifo wakipatikana na hatia.
Mahakama imeahirisha kesi hiyo kwa wiki mbili zijazo. Mpaka sasa washtakiwa wote wawili hawajakubali wala kukanusha mashtaka yanayowakabili.
Tangu kuanguka kwa miji ya Goma na Bukavu, ambayo ni miongoni mwa miji mikubwa iliyotekwa na waasi wa M23 mashariki mwa DR Congo, mamlaka za kijeshi zimewafikisha mahakamani maafisa kadhaa wa jeshi na polisi kwa tuhuma za uoga vitani.
Maafisa wengine waandamizi pia wanashikiliwa wakisubiri kusikilizwa kwa kesi zao.
0 Comments