
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameiomba Mahakama kutotegemea ushahidi uliotolewa na mashahidi wa kificho katika kesi inayomkabili, akidai kuwa baadhi ya ushahidi wao ulikuwa na uongo, mkanganyiko na maslahi.
Lissu ametoa ombi hilo leo, Jumatatu, Septemba 28, 2026, wakati akiendelea kuwasilisha hoja zake za mwisho mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.
Katika hoja zake, Lissu amewataja mashahidi hao kuwa ni PW5, PW7, PW8, PW10, PW11, PW13 na PW14, akidai kuwa ushahidi walioutoa mahakamani una mapungufu mbalimbali.
Lissu amesema ushahidi wa mashahidi hao haupaswi kupewa uzito kutokana na kile alichodai kuwa ni taarifa zisizo za kweli na zenye maslahi.
Kwa upande wa PW5, Lissu amedai kuwa shahidi huyo alitoa taarifa zinazokinzana kuhusu dini yake, akieleza kuwa mahakamani alikula kiapo kama Mkristo, wakati katika maelezo yake yaliyowasilishwa kama kielelezo D4 alijieleza kuwa ni Muislamu.
Pia amedai kuwa PW5 alitoa taarifa zisizo sahihi kuhusu uanachama wake wa CHADEMA.
Akizungumzia PW7, Lissu amedai kuwa shahidi huyo alitoa taarifa za uongo kuhusu kupelekwa katika Kituo cha Polisi Songea pamoja na suala la uanachama wake wa CHADEMA.
Kuhusu PW8, Lissu amesema ushahidi wake ulikuwa na mikanganyiko na taarifa ambazo, kwa mtazamo wake, hazikuwa za kweli.
Aidha, akielezea ushahidi wa PW10, Lissu amedai shahidi huyo alitoa maelezo kwa polisi kwamba mshtakiwa alisema walikuwa wamejipanga kufanya fujo ili kuzuia uchaguzi. Lissu amekanusha kauli hiyo, akisema hakuwahi kutoa kauli kama hiyo.
Kwa upande wa PW11, Lissu amesema ushahidi wake pia ulikuwa na mikanganyiko na kwamba haukuwa wa kweli.
Kuhusu PW13, Lissu amedai shahidi huyo alitoa taarifa zinazokinzana kuhusu uanachama wake wa CHADEMA, akisema katika maelezo yake alijitambulisha kama mwanachama wa chama hicho, jambo ambalo Lissu amepinga.
Lissu pia amepinga ushahidi wa PW14, akidai shahidi huyo alitoa taarifa zinazokinzana kuhusu kazi yake. Kwa mujibu wa Lissu, katika maelezo ya polisi shahidi huyo alijitambulisha kama mkulima wa Kata ya Mwakibete, huku mahakamani akisema yeye ni fundi umeme wa Jiji la Mbeya.
Lissu pia amekanusha madai kwamba PW14 alimsikia akisema “lazima tukichafue,” akisema hakuwahi kutoa kauli hiyo.
Hoja hizo zimewasilishwa na Lissu katika hatua ya hoja za mwisho, huku Mahakama ikiendelea kusikiliza pande zinazohusika kabla ya hatua inayofuata ya kesi.
0 Comments