Mhandisi Gabriel alitoa pongezi hizo alipolitembelea banda la VETA katika Maonyesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Manispaa ya Geita.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Gabriel alijionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na VETA na kuwataka vijana kutembelea banda hilo ili kujifunza fursa zinazotolewa na taasisi hiyo.
Amesema mapinduzi yanayofanywa na Serikali katika sekta mbalimbali ni makubwa, hivyo vijana wanapaswa kutumia fursa zinazopatikana VETA ili kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
“Ndoto na dhamira kubwa imebaki kwenye teknolojia ya madini. Nimeona VETA walivyo mabingwa, wanachukua vijana ambao wanapata ujuzi, wanajifunza VETA ili kujiajiri na kuajiriwa,” amesema Mhandisi Gabriel.
Amesema vijana wengi kwa sasa wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini, hivyo ni muhimu wapate mafunzo ya kitaalamu kupitia VETA ili kuongeza ufanisi na kutambulika kitaaluma.
“Watu waliopitia VETA wananufaika kupitia ujuzi walioupata, kwani wameandaliwa kupigana vita vya kiuchumi kupitia unyago wa teknolojia walioupata VETA,” amesema.
Aidha, amewataka Watanzania kutodharau elimu ya ufundi inayotolewa na VETA, akisisitiza kuwa dunia ya sasa imebadilika na inahitaji watu wenye ujuzi unaoendana na maendeleo ya teknolojia.
“Wito wangu kwa watu wa ndani ya Tanzania wasidharau VETA, waende wakasome, wapate ujuzi. Wasifikirie kufanya mambo kwa kubahatisha, kwa sababu dunia ya sasa imebadilika kupitia teknolojia mbalimbali,” amesema.
Amesema wahitimu wa VETA wana nafasi kubwa ya kutumia ujuzi wanaoupata katika kujiajiri au kuajiriwa, kutokana na mafunzo yanayolenga mahitaji ya soko la ajira na shughuli za uzalishaji.
Mhandisi Gabriel pia ameishauri VETA kuendelea kufanya tafiti na kuboresha mitaala na mafunzo yake ili yaendane na mahitaji ya teknolojia ya sasa na kuwawezesha vijana kunufaika zaidi na elimu ya ufundi.
“Ushauri wangu kwa VETA ni kuendelea kufanya utafiti na kuboresha elimu ya leo ili vijana waendelee kupata unyago wa teknolojia na kuzidi kunufaika kupitia VETA,” amesema.

0 Comments