Rais wa zamani wa Venezuela Nicolás Maduro na mkewe Cilia Flores, wameiomba mahakama ya Marekani kufuta mashtaka ya usafirishaji wa dawa za kulevya yanayowakabili.

Katika nyaraka zilizowasilishwa katika mahakama ya shirikisho ya Manhattan Jumatano, mawakili wao wamedai kuwa wana kinga dhidi ya mashtaka hayo kwa sababu Maduro alikuwa rais na Flores alikuwa mke wa rais.

Mawakili wa Maduro wamesema sheria za kimataifa haziruhusu mahakama za nchi moja kumfungulia mashtaka kiongozi wa nchi nyingine.

Flores anadai kuwa kinga hiyo inatokana na uhuru wa Venezuela na kwamba ni nchi hiyo pekee inayoweza kuiondoa.

Maduro na Flores wamekana mashtaka hayo.

Waendesha mashtaka wa Marekani wanasema Maduro na Flores walihusika katika mpango wa kusafirisha kwa magendo maelfu ya tani za kokeini kwenda Marekani, kwa kushirikiana na vikosi vya usalama vya Venezuela.

Iwapo watapatikana na hatia kwa makosa hayo, wanaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.Wawili hao wamezuiliwa Brooklyn tangu walipotekwa na vikosi vya Marekani katika operesheni iliyofanyika Caracas, Januari 1, 2026.

Marekani ilisema operesheni hiyo ilikuwa halali, lakini Maduro amesema hakuridhishwa nayo.Jaji Alvin Hellerstein atasikiliza hoja za pande zote mnamo Novemba 17. Kesi kuu imepangwa kuanza Juni 1, 2027, iwapo ombi lao litakataliwa