Takriban raia 7,000 wa Burundi wanaripotiwa kuwa wamerejea nchini kwao kufuatia msako dhidi ya wageni wanaoendesha biashara ndogo ndogo nchini Kenya, ulioanza mapema mwezi huu.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari wa wawakilishi wa taasisi za serikali siku ya Jumanne, Carine Nduwayo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Burundi alisema kuwa hadi sasa, wanaume 6,309, wanawake 593 na watoto 86 walio chini ya umri wa miaka mitano wamekwisharejea nchini.
Msako huo uliotarajiwa kuanza Septemba 7, kufuatia agizo la Rais William Ruto, ambaye katika mkutano aliokuwa amefanya awali alisema kuwa kuna baadhi ya biashara zilizokusudiwa kufanywa na Wakenya pekee.
Hata hivyo, baadaye serikali ya Kenya ilifafanua kuwa wageni wanaoendesha biashara kwa mujibu wa sheria wako huru kufanya biashara nchini humo.
Ufafanuzi huo ulitolewa baada ya mamia ya raia wa Burundi tayari kuanza harakati za kupata nyaraka za kusafiria, huku kukiwa na sintofahamu kuhusu iwapo wangeruhusiwa kuendelea kubaki nchini Kenya.
0 Comments