Tanzania imetoa wito wa kulindwa kwa raia, kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu bila vikwazo na kuhuishwa kwa juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kufikia amani ya kudumu katika Ukanda wa Gaza na Mashariki ya Kati.

Akihutubia Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Septemba 22, 2026, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania inaendelea kusisitiza umuhimu wa kupatikana kwa suluhisho la kudumu la mgogoro kati ya Israel na Palestina.

Ndejembi amesema Tanzania inaunga mkono suluhisho la nchi mbili, ambapo Israel na Palestina zitaishi pamoja kwa amani na usalama, kwa kuzingatia sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa.

Amesema Tanzania pia inatambua haki ya watu wa Palestina ya kujitawala, akisisitiza kuwa amani ya kudumu inapaswa kuzingatia utu, usalama na matarajio halali ya pande zote mbili.

Katika hotuba hiyo, Ndejembi ameeleza pia msimamo wa Tanzania kuhusu umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya nchi na sheria za kimataifa, huku akipinga hatua za upande mmoja zinazoweza kuathiri uchumi na ustawi wa wananchi wa nchi zinazolengwa.

Amesema Tanzania inaunga mkono ushirikiano wa kimataifa unaozingatia mamlaka ya kila nchi, huku ikihimiza kuondolewa kwa hatua zinazoweza kuwa kikwazo kwa maendeleo na utekelezaji kamili wa haki za binadamu.