Mamlaka na wakazi wa kaskazini mwa Tanzania wanapambana kuzima moto unaowaka kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika.

Moto huo unateketeza eneo lililoko katika mwinuko wa takriban mita elfu tatu na mia nne juu ya usawa wa bahari.

Afisa wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania ameiambia BBC kwamba bado haijafahamika kilichosababisha moto huo kuwaka.

Mlima Kilimanjaro, ambao ni muhimu kwa bioanuwai na utalii, umekumbwa na visa vingine vikubwa vya moto wa nyika viliyosababisha uharibifu katika miaka ya hivi karibuni.

Mwaka 2023, moto uliodumu kwa takriban wiki moja uliharibu eneo la kilomita 17 za mraba, sawa na takriban asilimia moja ya eneo la hifadhi ya mlima huo.