Marekani imekataa kumpa Rais wa Palestina Mahmoud Abbas visa ya kuingia nchini humo ili kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York wiki ijayo, vyanzo viwili vya Palestina vimeiambia BBC.
Hatua hiyo imekuja baada ya Marekani kusema inarefusha vikwazo vya visa dhidi ya maafisa wa Palestina, bila kumtaja Abbas, ikiwatuhumu kushindwa kutekeleza ahadi zao kuhusu mchakato wa amani.
Vikwazo hivyo vilianza kutekelezwa mwezi Agosti mwaka jana, wakati maafisa 80 wa Palestina waliponyimwa visa za kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa mjini New York.
Katika taarifa yake, Marekani iliishutumu Mamlaka ya Palestina (PA) na Shirika la Ukombozi wa Palestina (PLO) kwa "kutukuza ugaidi" na kujaribu "kupeleka mzozo wa Israel na Palestina kwenye ngazi ya kimataifa".
Mamlaka ya Palestina ilianzishwa kupitia makubaliano ya amani ya Oslo. Shirika la Ukombozi wa Palestina, lilitambuliwa baada ya mchakato huohuo kuwa mwakilishi rasmi wa watu wa Palestina, kwa masharti kwamba liitambue Israel na kukataa matumizi ya vurugu.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina iliviita vikwazo hivyo vya visa "hatua isiyo na uhalali ambayo inakwenda kinyume na juhudi za kujenga upya imani, kuimarisha uhusiano kati ya Palestina na Marekani, na kuunda mazingira muhimu ya kisiasa kwa ajili ya kutekeleza suluhisho la mataifa mawili na kufikia amani na utulivu".
Maafisa wa Palestina wamekana tuhuma za muda mrefu zinazotolewa na utawala wa Trump na Israel, wakisema wana haki ya kutafuta uwajibikaji dhidi ya dola inayokalia maeneo yao chini ya sheria za kimataifa.
Baada ya uamuzi wa visa wa mwaka jana, mwakilishi wa Abbas alisema hatua hiyo ilikuwa "kinyume waziwazi na sheria za kimataifa na Mkataba wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa".
0 Comments