Moto mwingine umeibuka katika Mlima Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania, wiki tatu tu baada ya moto mwingine uliodumu kwa karibu wiki mbili kudhibitiwa kwenye mlima huo wa juu zaidi barani Afrika.
Mamlaka za Tanzania zimesema moto huo ulianza alfajiri ya Jumatatu katika eneo la Sangarini, karibu na mwinuko wa Kamwanga, kuelekea Shira Plateau upande wa magharibi wa mlima huo.
Katika taarifa yake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Catherine Mbena, amesema timu ya pamoja inayojumuisha wazima moto, maafisa wa uhifadhi, wadau wa utalii na wananchi imepelekwa katika eneo hilo kudhibiti moto huo.
Mbena amesema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na uchunguzi unaendelea kubaini kilichosababisha tukio hilo.
Kwa mujibu wa mamlaka, moto huo unaendelea katika eneo la Shira Plateau lililo katika urefu wa takriban mita 3,800 kutoka usawa wa bahari, huku juhudi za kuuzima zikikabiliwa na changamoto ya upepo mkali na uoto unaowaka kwa urahisi.
Hata hivyo, mamlaka zimesema shughuli za utalii, ikiwemo upandaji wa Mlima Kilimanjaro, zinaendelea kama kawaida.
Mbena amesema kuanza kwa msimu wa mvua katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Tanzania kunatoa matumaini kwamba moto huo utaweza kudhibitiwa haraka.
Tukio hilo linajiri muda mfupi baada ya moto mwingine katika upande wa mashariki wa mlima huo kuteketeza zaidi ya hekta 1,800 za uoto wa asili kabla ya kudhibitiwa. Wakati huo, mamlaka zilieleza kuwa shughuli za kibinadamu huenda zilichangia kuzuka kwa moto huo.
0 Comments