SERIKALI imeahidi kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya bidhaa za uzazi wa mpango kwa angalau asilimia 10 kila mwaka, ikiwa ni hatua ya kuimarisha huduma za afya ya uzazi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Ahadi hiyo ilitolewa Septemba 28,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uzazi wa Mpango Duniani na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Wizara ya Afya, Ziada Sellah, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Grace Magembe.

Sellah alisema uzazi wa mpango ni uwekezaji muhimu katika afya ya watu, ustawi wa familia na maendeleo ya Taifa, kwa kuwa unaziwezesha familia kufanya maamuzi kuhusu idadi ya watoto na muda wa kupanga kati ya uzazi mmoja na mwingine.

“Ahadi ya Tanzania ya Uzazi wa Mpango 2030 inatoa msingi muhimu wa kuimarisha ufadhili endelevu wa ndani wa uzazi wa mpango, ikiwa ni pamoja na kuongeza rasilimali za ndani kwa ajili ya bidhaa za uzazi wa mpango kwa angalau asilimia 10 kila mwaka na kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatolewa kikamilifu,” alisema.

Alisema kuongeza uwekezaji katika uzazi wa mpango kutasaidia pia kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan Lengo la Tatu linalohusu afya bora na ustawi.
Naibu Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Melissa McNeil-Barrett, alisema uzazi wa mpango haupaswi kuangaliwa kwa upande wa upatikanaji wa bidhaa na huduma pekee, bali pia kuhakikisha watu wanapata taarifa sahihi na wanaweza kufanya maamuzi yenye uelewa kuhusu afya yao ya uzazi.

“Uzazi wa mpango hauhusu tu upatikanaji wa bidhaa na huduma. Pia ni kuhakikisha watu wanapata taarifa sahihi, wanaweza kupata huduma hizo na wako huru kufanya maamuzi yenye uelewa kuhusu afya yao ya uzazi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MSI Tanzania, Patrick Kinemo, alisema mabadiliko katika ufadhili kutoka kwa wafadhili yameongeza umuhimu wa Serikali kuimarisha uongozi, ushirikiano na umiliki wa kitaifa katika kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kupatikana.

Alisema uzazi wa mpango ni sehemu muhimu ya afya ya mama, mtoto mchanga na afya ya uzazi, huku akibainisha kuwa huduma hizo za hiari zinaweza kuchangia ujauzito wenye afya na kupunguza vifo vya akina mama vinavyoweza kuzuilika.

Kinemo alisema bado kuna vikwazo vinavyoathiri upatikanaji wa huduma hizo, ikiwamo ukosefu wa taarifa, taarifa potofu, changamoto za kifedha na kijiografia pamoja na vikwazo vya kijamii na ndani ya mfumo wa afya.

Alisema washirika wanaendelea kushirikiana na Serikali kusogeza huduma karibu na jamii, hususan maeneo ya pembezoni, pamoja na kujenga uwezo wa wahudumu wa afya na kuboresha ubora na upatikanaji wa huduma.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya “Hakuna Vikwazo, Chaguo Pekee” inalenga kuhimiza upatikanaji wa taarifa sahihi, huduma bora na chaguo mbalimbali za uzazi wa mpango kwa wanawake, wasichana, vijana, wanandoa na watu binafsi.

Siku ya Uzazi wa Mpango huadhimishwa duniani kote Septemba 26 kila mwaka kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu uzazi wa mpango na kuwawezesha watu kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya yao ya uzazi.

Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv