
TANGA: WANAWAKE na watoto katika Kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wameanza kupata fursa mpya za elimu na uwezeshaji wa kijamii, hatua inayolenga kuwasaidia kujenga maisha bora katika mazingira yao mapya.
Mabadiliko hayo yanaenda sambamba na jitihada za Shirika lisilo la Kiserikali la Mimute Women Organization, kwa kushirikiana na uongozi wa eneo hilo, kuhakikisha wanawake na watoto wanapata fursa za elimu na huduma nyingine muhimu za kijamii.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Rose Njilo, alisema elimu ni msingi wa maisha na kwamba uwezeshaji wa wanawake na watoto ni muhimu katika kujenga jamii yenye uwezo wa kujitegemea na kutumia fursa zinazopatikana katika eneo hilo.
Alisema shirika hilo limeamua kuweka msukumo mpya katika elimu kwa kutambua changamoto zinazowakabili wananchi wa Msomera na kushirikiana na Serikali pamoja na viongozi wa eneo hilo kuzitafutia ufumbuzi.
Njilo alisema ziara yao pia imelenga kujionea hali halisi ya maisha ya wananchi na kutathmini namna wanawake na watoto wanavyoweza kunufaika zaidi na fursa zilizopo.
Alisema tayari watoto wanane wameanza kupata msaada, ikiwa ni hatua ya kwanza ya shirika hilo katika kuwawezesha watoto wanaohitaji msaada wa kielimu.
Aidha, aliwataka viongozi wa eneo hilo kushirikiana na Mimute kubaini familia zenye watoto wanaohitaji msaada, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

Njilo alisema shirika hilo pia linaangalia uwezekano wa kusaidia vikundi viwili au vitatu vya wanawake, ikiwamo vikundi vya kuweka na kukopa, ili kuwaongezea uwezo wa kiuchumi na kuwasaidia kujitegemea.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Musima, Morisa Melubo, alisema wananchi waliokuja Msomera kutoka maeneo mbalimbali, wakiwamo waliotoka Ngorongoro, wameanza kujenga maisha mapya kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Alisema awali maisha ya wananchi wengi yalitegemea zaidi ufugaji, lakini baada ya kufika Msomera wameanza kujihusisha na kilimo, biashara, usafirishaji wa bodaboda, maduka na shughuli nyingine za uzalishaji.
Melubo alisema uwepo wa wataalamu na ushauri kutoka Serikali umeendelea kuwasaidia wananchi kuendana na mazingira mapya ya maisha na uzalishaji.
Alisema Msomera pia imeendelea kupata maendeleo katika sekta za elimu, afya, barabara na maji, huku eneo hilo likiwa na zaidi ya barabara 50 za ndani pamoja na barabara kuu zinazounganisha maeneo mbalimbali.
Alisema baadhi ya wanafunzi wameonyesha uwezo katika maeneo mbalimbali na kupata nafasi katika shule za vipaji maalum, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau katika kuongeza fursa kwa wananchi.
Melubo alisema ni muhimu Mimute na Serikali ya eneo hilo kuendelea kukaa pamoja na kubaini maeneo yenye uhitaji mkubwa ili rasilimali zinazopatikana zitumike kwa ufanisi na kuwasaidia wananchi kujenga maisha bora
0 Comments