Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema nchi yake haitasalimu amri wala “kupiga magoti” mbele ya shinikizo kutoka Marekani, akitoa kauli hiyo wakati akihutubia Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York.

Pezeshkian amesema Iran itaendelea kupinga vikwazo, shinikizo na kile alichokiita vitisho dhidi ya nchi yake, akimlenga Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye siku moja kabla alitoa kauli kuhusu uwezekano wa kuchukua hatua kali dhidi ya Iran huku akisema mazungumzo kati ya Washington na Tehran yanaendelea.

Katika hotuba yake, Pezeshkian aliishutumu Marekani kwa kile alichokiita “ugaidi”, akirejea kuuawa kwa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, mwanzoni mwa vita. Pia alionyesha picha ya Khamenei pamoja na picha za watoto wa shule wa Iran waliouawa katika siku za mwanzo za mashambulizi.

Rais huyo amesisitiza kuwa Iran haikuanza vita na kwamba nchi yake ilichukua hatua za kujilinda dhidi ya mashambulizi kutoka Marekani na Israel.

“Upinzani wa watu wa Iran utaongezeka tu mbele ya vikwazo, shinikizo na vitisho vinavyoongezeka. Hatutainamisha vichwa vyetu wala kupiga magoti,” Pezeshkian alisema.

Pezeshkian pia amezungumzia Mlango wa Hormuz, akisema Tehran haitaruhusu njia hiyo ya kimkakati ya usafirishaji wa mafuta itumike kama chombo cha mashambulizi dhidi ya Iran.

Amesema Iran haiwezi kuruhusu baadhi ya nchi kutumia njia hiyo kwa uhuru na kunufaika nayo huku ikitumiwa pia kuendeleza kile alichokiita uchokozi dhidi ya nchi yake.

Licha ya msimamo huo mkali, Pezeshkian amesema Iran iko tayari kwa mazungumzo na diplomasia, lakini si mazungumzo yanayoendeshwa kwa lugha ya vitisho au matumizi ya nguvu.

Hotuba hiyo imekuja siku moja baada ya Trump kuhutubia UN na kueleza msimamo wake kuhusu Iran, huku akitaja pia uwezekano wa makubaliano kati ya Marekani na Tehran. Kauli hizo zinafuatia kipindi cha mvutano mkubwa kati ya pande hizo kuhusu vita na masuala mengine ya usalama katika eneo hilo.