Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Antiphas Lissu, leo Septemba 23, 2026 ameendelea na mawasilisho yake ya mwisho katika Mahakama Kuu ya Tanzania, akieleza hoja mbalimbali za kisheria na kiushahidi anazoomba mahakama izingatie katika uamuzi wa kesi ya uhaini inayomkabili.

Katika mawasilisho hayo, Lissu amesisitiza kuwa hakatai kwamba aliwahi kutoa maneno yanayodaiwa kuwa sehemu ya shtaka, akisema hoja yake ya msingi ni iwapo maneno hayo yanatosha kisheria kuunda kosa la uhaini au kosa lingine la jinai. Amesema kauli hizo zilitolewa katika nyakati na maeneo mbalimbali nchini na hazikuwa siri.

Lissu amesema kesi hiyo ni ya tatu ya uhaini kufunguliwa nchini Tanzania, lakini ametofautisha kesi hiyo na kesi mbili zilizotangulia mwaka 1970 na 1983, akisema kesi hizo zilihusu madai ya jaribio la kupindua Serikali na kumuua Rais. Kwa mujibu wa mawasilisho yake, kesi yake inahusu madai ya kutishia Serikali, hivyo uamuzi wa mahakama unaweza kuweka msingi wa kisheria kuhusu tafsiri na matumizi ya kosa hilo katika siku zijazo.

Akifafanua kifungu cha sheria kinachotumika katika mashtaka yake, Lissu amesema kuna masharti kadhaa ambayo upande wa mashtaka unapaswa kuyathibitisha, ikiwemo kuwepo kwa nia ya kutenda kosa la uhaini, nia ya kuchochea mtu au kikundi cha watu, pamoja na kuoneshwa kwa nia hiyo kupitia uchapishaji au njia nyingine inayotambuliwa na sheria. Pia ameeleza kuwa, kwa tafsiri yake ya sheria, matokeo yaliyolengwa na nia hiyo yanapaswa kuoneshwa.

Lissu pia amerejea kanuni za kisheria zinazohusu uhaini, akisema moja ya masharti muhimu ni kuthibitishwa kwa kitendo cha wazi na si kutegemea maneno pekee. Ameeleza kuwa katika mazingira fulani maneno hayawezi kuchukuliwa kuwa kitendo cha wazi cha uhaini isipokuwa yawe yanaelezea matendo yanayohusiana na kosa hilo.

Katika hoja nyingine, Lissu amepinga madai kwamba ndiye aliyeitisha mkutano wa CHADEMA wa Aprili 3, 2025, akisema hakuna hata mmoja kati ya mashahidi 17 wa upande wa mashtaka aliyetoa ushahidi wa namna mkutano huo ulivyoitishwa. Ameirejea pia hoja ya mashahidi wa utetezi, akiwemo John Mnyika, ambao walieleza kuwa mkutano uliandaliwa na Sekretarieti ya CHADEMA na kwamba Lissu pamoja na John Heche walikuwa miongoni mwa walioalikwa.

Kuhusu madai kwamba aliwaalika waandishi wa habari kwenye mkutano huo, Lissu ameyapinga akirejea ushahidi wa upande wa utetezi kwamba waandishi walialikwa na Brenda Rupia. Amesema ushahidi huo uliungwa mkono na mashahidi wengine wa utetezi na kwamba haukuhojiwa na upande wa mashtaka.

Hoja nyingine aliyoiwasilisha ni kuhusu matumizi ya neno “umma” katika shtaka. Lissu amesema kifungu cha sheria kinachotumika kinataja kuchochea mtu au kikundi cha watu kuitishia Serikali, wakati hati ya mashtaka inamtuhumu kuchochea umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Kwa msingi huo, amehoji uhalali wa shtaka hilo na kudai kuwa sheria haijaweka kosa la “kuchochea umma” kama linavyoelezwa katika mashtaka yake.

Lissu pia amerejea Ibara ya 13(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu kutoadhibiwa kwa kitendo ambacho hakikuwa kosa chini ya sheria wakati kilipofanyika. Amesema kwa kuzingatia msingi huo, anaamini mahakama inapaswa kuangalia kwa umakini kama kitendo anachotuhumiwa nacho kimeainishwa wazi kuwa ni kosa katika sheria.

Mawasilisho hayo yanaendelea katika hatua ya mwisho ya kesi, huku Lissu akiomba majaji kuzingatia hoja zake za kisheria pamoja na ushahidi uliotolewa na pande zote kabla ya kutoa uamuzi.

Lissu: Waheshimiwa majaji, kifungu cha 39(2)(d) cha sheria iliyotumika kunishtaki kinasema: “Mtu yeyote anayechochea mtu au kikundi cha watu…”

Shtaka dhidi yangu linasema nimechochea umma. Kwenye kifungu hicho cha 39(2) hakuna umma, kuna mtu au kikundi cha watu.

Sasa umma ni nini? Hiki kitu kinachoitwa umma ni kitu gani?

Kanuni ya Adhabu imetoa tafsiri ya neno umma. Tafsiri ya umma kwa mujibu wa sheria hii ina maana ya watu wote wa Tanzania Bara bila kujali uraia wao. Kila mtu aliyeko ndani ya mipaka ya Tanzania Bara, pamoja na watu wanaokaa mahali popote au wanaotumia sehemu yoyote, mfano baa, gesti au vilabu. Ni idadi yoyote ya watu, hata watu ambao hata ufanyeje huwezi kuwajua.

Huo ndio umma ambao ninatuhumiwa kuuchochea ili uzuie uchaguzi.

Sheria niliyoshitakiwa nayo inasema unachochea mtu au kikundi cha watu. Mtu anajulikana. Lakini kikundi cha watu ni nini hasa?

Natumia Oxford Advanced Learner’s Dictionary. Kikundi ni idadi ya watu au vitu ambavyo vipo pamoja katika sehemu moja au vinaunganishwa kwa namna fulani.

Hiyo ndiyo maana ya kikundi.

Si watu wote. Watu wote hawawezi kuwa kikundi. Kikundi ni sehemu ya watu wote.

Nimeshtakiwa kwa kitu ambacho hakipo kwenye sheria.

Sheria iko wazi kabisa.

Lissu: Waheshimiwa majaji, hili kosa lilivyoletwa, hizi taarifa zilivyoletwa, haziwezi kujibika.

Hakuna mtu anayeweza kujitetea kwa hati kama hii, kuambiwa umechochea watu wote, waliopo uwanja wa ndege na waliopo majumbani kwao.

Hilo halipo kwenye kifungu cha sheria ya Kanuni ya Adhabu niliyoshitakiwa nayo.

Waheshimiwa majaji, kwa sababu ya upana wa hilo neno umma, upande wa mashtaka ulikuwa na wajibu wa kisheria kueleza huo umma ni upi katika hati yao ya mashtaka ili kumwezesha mshtakiwa kuandaa utetezi wake.

Upande wa mashtaka ulitakiwa kueleza huo umma unaodaiwa kuchochewa.

Hawakufanya hivyo.

Wameleta kitu ambacho hakipo kwenye sheria.

Basi turudi kwenye misingi.

Nilisema kitu kinachoitwa kosa la jinai ni kile kilichokatazwa na sheria. Ni kitendo.

Kifungu cha 39(2) kimetengeneza kosa la uhaini kwa mtu yeyote anayechochea mtu au kikundi cha watu kuitishia serikali.

Sheria haijatengeneza kosa la mtu kuchochea watu wote, yaani umma.

Hakuna sheria ya namna hiyo.

Hakuna sheria inayosema ukichochea watu wote ni kosa.

Sheria inasema ukichochea mtu au kikundi cha watu.

Nimeshtakiwa. Nipo gerezani kwa mwaka mmoja na nusu sasa kwa kitu ambacho hakipo kwenye sheria za nchi hii.

Ibara ya 13(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema:

“Ni marufuku kwa mtu kuadhibiwa kwa kitendo chochote ambacho alipokifanya hakikuwa kosa chini ya sheria.”

Nimeshtakiwa kwa kuchochea umma.

Hakuna sheria inayoitwa kuchochea umma.

Kuna sheria inayosema kuchochea mtu au kikundi cha watu.

Nimeshtakiwa kwa kitendo ambacho wala si kosa.

Lissu: Hoja yangu ni kwamba, kwa sababu migongano hiyo inahusu jambo kubwa linalohusu ushahidi wa kwamba mshtakiwa aliwaalika au hakuwalika waandishi wa habari, inaonesha kwamba ushahidi huo hauna thamani yoyote.

Vipi kuhusu ushahidi wa utetezi kwenye hoja hii? Unasemaje?

Ushahidi wa utetezi umefuta shaka yoyote kuhusu mshtakiwa kuwaalika waandishi wa habari kwenye mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025.

Kama kulikuwa na shaka kwamba mshtakiwa aliwaalika waandishi wa habari, imeondolewa yote na ushahidi wa utetezi.

Sisi tunasema kwamba waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025 walialikwa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, bila shaka yoyote. Wote wamesema hivyo.

Ushahidi huu upo katika ukurasa wa 592. Ushahidi wa DW2 upo katika ukurasa wa 621 hadi 622. Ushahidi wa DW3 upo katika ukurasa wa 693. Ushahidi wa DW4 upo katika ukurasa wa 800.

Mashahidi hao wote wanne wamesema kwamba aliyewaalika waandishi wa habari ni DW4, Brenda Rupia.

Waheshimiwa majaji, ushahidi huo haukuhojiwa hata mara moja.

Sasa, nini maana ya kutokuhojiwa kwa ushahidi huu?

Lissu: Kwa sababu hizi, jibu la swali la pili, je, mshtakiwa aliwaalika waandishi wa habari kwenye mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025, jibu lake ni hapana.

Hiyo ni kusema kwamba mshtakiwa hakuwalika waandishi wa habari kwenye mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025.

Swali la tatu ni hili: Je, mshtakiwa alitengeneza nia ya kuchochea mtu yeyote au kikundi cha watu kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Kwa kesi hii, hili ni suala la kufa au kupona, kwa sababu ni moja ya mambo muhimu zaidi katika kesi nzima dhidi yangu.

Taarifa iliyopo mahakamani inayonishtaki inanituhumu kwamba nilitengeneza nia ya kuhamasisha umma na kuchochea umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hiyo ndiyo tuhuma.