KAHAMA: Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, ametoa maagizo kwa wamiliki na mameneja wa migodi nchini kuhakikisha wanaboresha maeneo ya uchimbaji wa madini, hususan upande wa maduara, uwekaji wa mtingi na vyoo, ili kuhakikisha usalama kabla ya mvua za El Nino zinazotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuanza kunyesha.

Mhandisi Samamba ametoa maagizo hayo leo alipokuwa mgeni rasmi katika semina ya wachimbaji wadogo iliyolenga maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua za El Nino katika maeneo ya uchimbaji wa madini.

Amesema maagizo hayo yanaendana na msisitizo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wa kuchukua tahadhari mapema na kuhakikisha miundombinu katika maeneo ya uchimbaji inakuwa salama.

Mhandisi Samamba amesema asilimia 70 ya ajali zote migodini zinatokana na udongo kulowana na kuwa mzito, huku mtingi ukiwa wa muda mrefu na wakati mwingine kuoza, hivyo jitihada za kuboresha miundombinu zinapaswa kuanza mapema ili kuepusha vifo na madhara kwa wachimbaji.

“Mojawapo ya majanga yanayosababisha vifo vya watu wengi ni ajali za migodini, lakini tukijitahidi kutengeneza miundombinu mizuri, mfano kuweka mifereji itakayosaidia kutiririsha maji, kubadilisha mtingi na kuweka wenye ubora pamoja na kujenga vyoo vizuri ili kuepuka magonjwa kama kipindupindu, tutapunguza madhara,” amesema Mhandisi Samamba.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA), ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Madini Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), Gregory Kagusi, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wachimbaji kwa kuwa yanawawezesha kuelewa athari zinazoweza kusababishwa na mvua zinazotarajiwa.

Amesema wachimbaji watahakikisha wanazingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali ili kujilinda na madhara yanayoweza kutokea wakati wa mvua hizo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wakaguzi wa Migodi Tanzania (CHAWUMITA), Shija Musa, amesema wameanza kuchukua hatua za tahadhari kwa kufunga mtingi na kufukia mashimo ambayo hayatumiki.

Amesema chama hicho kitaendelea kuhakikisha maelekezo yote yanayotolewa na Serikali kuhusu usalama wa wachimbaji yanatekelezwa