MISSENYI: Vitendo vya uchomaji moto misitu, mashamba na maeneo ya malisho vimeendelea kuleta hofu na simanzi kwa wawekezaji na wananchi katika Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera, huku wadau wakihimiza kuongezwa kwa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya uchomaji moto.

Mwekezaji wa shamba la kilimo cha kahawa na migomba la Bwikaranyange Investment Ltd, lililopo Kata ya Bugandika wilayani Missenyi, ameiomba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kupitia Kitengo cha Majanga kuongeza kasi ya utoaji elimu kuhusu madhara ya uchomaji moto misitu na maeneo mengine.

Mwekezaji huyo, Justine Lambart, kupitia Meneja wa shamba hilo, Optat Rwebugisa, amesema uwekezaji huo una thamani ya Sh milioni 600, ambapo tayari uwekezaji umefanyika katika eneo lenye ukubwa wa ekari 374 kati ya ekari 570.

Amesema changamoto ya uchomaji moto imekuwa kikwazo kikubwa kinachozua taharuki katika maandalizi ya uwekezaji na mipango ya baadaye ya kujenga kiwanda katika eneo hilo.

Rwebugisa amesema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kupitia Kitengo cha Majanga inapaswa kubadili mbinu na mipango ya utoaji elimu kuhusu madhara ya kuchoma nyika, mashamba na maeneo ya malisho ya mifugo, akieleza kuwa katika msimu wa kiangazi maeneo makubwa yanayochomwa moto yanaweza kugeuka kuwa majanga makubwa.

Amesema hali hiyo pia inaweza kukatisha tamaa wawekezaji wanaokusudia kuwekeza katika Wilaya ya Missenyi.

“Tangu nimeanza kufanya uwekezaji, tishio la moto katika eneo letu limekuwa endelevu. Mara nyingi shughuli za uwekezaji zinasitishwa kwa ajili ya kuhangaika kuzima moto katika eneo letu na maeneo ya jirani, huku chanzo cha moto huo kikiwa hakijulikani,” amesema.

Amesema hivi karibuni moto ulichoma mashamba ya jirani na kuhatarisha nyumba pamoja na Shule ya Sekondari Bwabuki, huku shule hiyo ikinusurika.

Ameongeza kuwa kuna wakati moto ulichoma shamba la miti katika eneo lao, huku siku nyingine wafanyakazi na vibarua wakilazimika kusitisha shughuli zao kwa takribani saa tano ili kwenda kuzima moto katika mashamba ya jirani.

“Kama mnavyoona, shamba hili limetandazwa mabomba kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Kama moto utaunguza shamba, hasara inaweza kuwa kubwa. Mara nyingi wanasema wanaochoma mashamba ni wafugaji, lakini je, kweli elimu kuhusu kuchoma misitu au maeneo ya kufugia imetolewa?” amehoji Rwebugisa.

Amesema hali hiyo imeifanya tishio la moto kuwa jambo linalowafanya wawekezaji kuwa na hofu kuhusu usalama wa mali na uwekezaji wao.

Madai hayo yameibuka siku chache baada ya Jeshi la Polisi kutoa taarifa kwamba vijana wa shamba la mwekezaji waliokuwa wakisafisha eneo kwa ajili ya kupanda migomba na mibuni walidaiwa kusahau kuzima moto na kusababisha mashamba ya majirani kuungua.

Hata hivyo, baada ya vyombo vya habari kufika katika shamba hilo, uongozi wa shamba ulisema mashamba ya miti yaliyoungua yalikuwa mbali na eneo la uwekezaji, yakiwa katika kata jirani, na kwamba Jumapili si siku ya kusafisha shamba bali ni siku ya shughuli za umwagiliaji.

Msimamizi wa Umwagiliaji katika shamba hilo, Majaliwa Patrick, amesema waliona moto ukiwaka katika mashamba ya Kata ya Kitobo, kata jirani, hivyo wafanyakazi na vibarua walitoa nguvu zao kwenda kuzima moto huo.

Amesema hakuna kipande cha shamba la Bwikaranyange Investment kilichoungua siku hiyo, huku akieleza kuwa Jumapili ambayo Jeshi la Polisi lilisema moto ulitokea, ilikuwa siku ya mapumziko katika eneo hilo la uwekezaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, mashamba 39 ya watu watano yenye thamani ya Sh milioni 36.9 katika Kijiji cha Kijunja, Kata ya Kitobo wilayani Missenyi, yaliungua baada ya vijana wanne kuwasha moto kwa ajili ya kusafisha shamba katika eneo la mwekezaji lililopo Kata ya Bugandika na kusahau kuuzima.

Hata hivyo, Chatanda alisema vijana hao hawakuwa wamefahamika majina hadi wakati huo, huku akiwataka wananchi kuacha vitendo vya kuchoma moto misitu na mashamba.

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Mstaafu Hamis Mahiga, amesema moto kwa wawekezaji katika wilaya hiyo ni tishio kubwa linaloendelea kuleta maumivu kwa wawekezaji na wananchi wa kawaida.

Amesema katika msimu wa kiangazi kila mwaka, maeneo ya nyika na misitu katika wilaya hiyo huchomwa kwa kiwango kikubwa, akieleza kuwa mwaka huu hata mashamba makubwa ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yameungua.

Ameongeza kuwa mashamba ya wananchi, wawekezaji wa kilimo cha miwa, miundombinu na baadhi ya nyumba pia viliungua na kusababisha simanzi kwa wananchi.

Mahiga amesema uongozi unaendelea kuchunguza chanzo cha uchomaji moto huo, huku akieleza kuwa hata wafugaji wanaodaiwa kuchoma moto mara nyingi hawasikiki wakiacha ushahidi unaoweza kusaidia kuwabaini na kuwachukulia hatua.

Ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano katika kukabiliana na majanga ya moto, akisema uchomaji moto una madhara mbalimbali, ikiwemo kuharibu miundombinu ya umeme, shule na misitu, pamoja na kuchangia athari za mabadiliko ya tabianchi.