SHINYANGA: MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amezindua kampeni ya usafi wa mazingira kila Jumamosi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha usafi katika mikoa yote nchini.

Kampeni hiyo imezinduliwa leo, Septemba 25, 2026, kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Soko la Ibinzamata lililopo

Manispaa ya Shinyanga, ikiwa pia ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua za El Niño kwa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhita amesema usafi wa mazingira haupaswi kuonekana kuwa jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi katika maeneo anayoishi na kufanyia shughuli zake.

Amesema nidhamu ya usafi inaanzia kwa mtu binafsi, ikiwemo kusafisha maeneo yanayomzunguka, mitaro na mazingira ya makazi yake ili kuzuia uchafuzi wa mazingira.

“Usafi ni jukumu la kila siku na ni nidhamu. Unapokuwa na nidhamu ya usafi, ndipo unapowaza kusafisha kibaraza chako na mitaro ya mtaani kwako. Kila mmoja kwenye ngazi zote za uongozi tukawajibike ili tulete mabadiliko chanya,” amesisitiza Mhita.

Aidha, Mhita amesema Manispaa ya Shinyanga imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kwa miaka mitatu mfululizo katika suala la usafi, hivyo kuna umuhimu wa kuboresha zaidi mienendo na mikakati ya usafi ili kuendelea kufanya vizuri.

Amesema mkakati wa kuimarisha usafi katika mkoa huo ni kutekeleza maelekezo ya Rais Samia ya kufanya kila Jumamosi kuwa siku ya usafi, kwa kushirikisha wananchi na viongozi katika ngazi zote.

Amehimiza wananchi kujenga utamaduni wa kufanya usafi mara kwa mara na kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi, hatua itakayosaidia kuboresha afya za jamii na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.