TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Doha Dialogue kuhusu uhamaji wa nguvu kazi na ajira, utakaofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam, ukiwa ni mkutano wa kwanza kufanyika ndani ya bara la Afrika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, alisema kuwa mkutano huo utatoa fursa kwa Tanzania kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika na GCC+ katika masuala ya uhamaji wa nguvu kazi na ajira.

Mkutano huo utawakutanisha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba (GCC+), ambazo ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain, pamoja na Jordan na Lebanon.

Sangu alisema mkutano huo ni jukwaa la kimataifa linalolenga kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa uhamaji wa nguvu kazi na kukuza ajira zenye staha, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Na katika mkutano huu mkuu kabisa, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Daktari Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Alisema Mkutano wa Kwanza wa Doha Dialogue ulifanyika jijini Doha, Qatar, Mei 21 na 22, 2024, ukihusisha nchi 33, ikiwemo nchi 25 za Afrika, nchi za Ghuba pamoja na Jordan na Lebanon, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zilizoshiriki.

Kwa mujibu wa Sangu, mkutano huo ulipitisha azimio lililoitwa Doha Declaration, lililoweka msingi wa kuendeleza majadiliano na ushirikiano kati ya nchi za Afrika na nchi za Kiarabu kuhusu uhamaji wa nguvu kazi.

“Tanzania ni nchi ya pili kuwa mwenyeji wa Doha Dialogue, mkutano huu ambao unafanyika kila baada ya miaka miwili. Na kwa mara ya kwanza ndio unafanyika ndani ya bara la Afrika,” alisema.

Alisema maeneo muhimu yatakayojadiliwa ni pamoja na uimarishaji wa mikataba ya ajira baina ya nchi, uoanishaji wa ujuzi wa wafanyakazi na mahitaji ya soko la ajira na ujenzi wa mifumo ya uhamaji wa nguvu kazi inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, mahitaji mapya ya soko la ajira na kazi zenye staha.

Sangu alisema mkutano huo pia utatoa fursa kwa Tanzania kuimarisha nafasi yake katika mijadala ya kimataifa kuhusu uhamaji wa nguvu kazi, kupanua fursa za ajira nje ya nchi, kulinda haki za wafanyakazi na kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika na GCC+.

“Mkutano huu pia utaongeza ushindani wa nguvu kazi ya Tanzania na kuchangia katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050,” alisema.

Alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kupitia balozi pamoja na kuwa na siku maalum za kukutana na Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi ili kupata mrejesho kuhusu mazingira yao ya kazi.


Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv