Tanzania imeitaka Jumuiya ya Kimataifa kuongeza juhudi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan kupanda kwa kina cha bahari, kwa kuongeza upatikanaji wa fedha za tabianchi, teknolojia na mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema.

Akizungumza katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kupanda kwa kina cha bahari, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi, amesema changamoto hiyo si tishio la baadaye pekee, bali tayari inaathiri maisha ya watu, uchumi na mazingira katika maeneo mbalimbali duniani.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoweza kuathirika kutokana na kuwa na ukanda mpana wa pwani ya Bahari ya Hindi, pamoja na Zanzibar na visiwa vingine vinavyotegemewa na mamilioni ya watu kwa shughuli za uvuvi, utalii na biashara.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, baadhi ya athari zinazoshuhudiwa ni pamoja na mmomonyoko wa fukwe, kuingia kwa maji ya chumvi kwenye vyanzo vya maji baridi na mafuriko, hali ambayo inaweza kuathiri wananchi, miundombinu na mafanikio ya maendeleo.

Amesema Tanzania tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kuimarisha ulinzi wa maeneo ya pwani, kurejesha mikoko na mifumo ya ikolojia, kuimarisha usalama wa maji pamoja na kuendeleza mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inayoshirikisha jamii.

Hata hivyo, amesema juhudi za nchi moja moja haziwezi kutosha kukabiliana na ukubwa wa changamoto hiyo.

Makamu wa Rais ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinapatikana kwa kiasi cha kutosha, kwa uhakika na kwa urahisi zaidi, hasa kwa nchi zinazoendelea na jamii za pwani zilizo katika mazingira hatarishi.

Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa umewakutanisha viongozi, nchi wanachama, wataalamu na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili hatua za pamoja za kukabiliana na athari za kupanda kwa kina cha bahari na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Mjadala huo unaendelea kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi, kufuatia mkutano wa ngazi ya juu uliofanyika mwaka 2024 ambao uliweka suala la kupanda kwa kina cha bahari katika mjadala mpana wa kimataifa.