Serikali ya Uganda imetoa wito wa kutatuliwa kwa migogoro na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati kupitia mazungumzo ya amani.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu na Wizara ya Mambo ya Nje, Uganda imesema haungi mkono vita visivyo na msingi.

Serikali hiyo imezitaka pande zote kutambua uwepo wa Israel kama taifa, huku ikiunga mkono haki ya Wapalestina kuwa na taifa lao.

Uganda imesema sehemu kubwa ya matatizo ya eneo hilo inatokana na kushindwa kushughulikia ipasavyo suala hilo kwa muda mrefu.

Kuhusu matumizi ya nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani, Uganda imesema suala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia sheria za kimataifa.

Serikali hiyo pia imekosoa siasa zinazotegemea ukabila na dini, ikizielezea kama “sumu” inayoweza kuathiri jamii na mustakabali wa nchi.