Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman maarufu OMO, leo Septemba 22, 2026, ameapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Othman ameapishwa katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Zanzibar na kuongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, huku ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa.
Uapisho huo umefanyika kufuatia makubaliano yaliyofikiwa katika mchakato wa maridhiano ya kisiasa Zanzibar, ambapo Othman aliteuliwa kushika nafasi hiyo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa uapisho huo, Othman anaanza rasmi kutekeleza majukumu ya nafasi hiyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya maridhiano na ushirikiano wa kisiasa Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman maarufu OMO, amesema kukamilika kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) si mwisho wa safari kwa wananchi wa Zanzibar, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya kujenga ukweli, ushirikiano na mshikamano.
Othman amesema mchakato huo hauhusu viongozi au vyama vya siasa pekee, bali ni safari ya wananchi wote katika kujenga Zanzibar wanayoitaka.
Akizungumza leo, Septemba 22, 2026, baada ya kuapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman amesema maridhiano hayapaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa maslahi ya vyama pekee.
Amesema yanapaswa pia kuzingatia mabadiliko yanayoendelea duniani, ikiwemo maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.
Othman amesema dunia inapitia mageuzi makubwa na kwamba baadhi ya nchi zimepiga hatua kupitia sera nzuri na maendeleo katika sekta mbalimbali.
Amesema Zanzibar inapaswa kujiuliza namna ya kutumia mabadiliko hayo na fursa zinazojitokeza duniani kwa manufaa ya wananchi wake.
Hii ni mara ya pili kwa Othman kushika nafasi hiyo. Alihudumu kama Makamu wa Kwanza wa Rais kuanzia mwaka 2021 hadi 2025, kabla ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya kipindi hicho kumalizika baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.
Othman, ambaye ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, aliteuliwa tena na Dk Mwinyi baada ya chama hicho kumteua kwa nafasi hiyo. Chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ACT-Wazalendo inapata nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kutokana na kuwa chama cha pili kwa kura katika uchaguzi wa urais.
Kabla ya kuingia katika siasa za upinzani, Othman alikuwa na historia ndefu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, akiwahi kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Mwaka 2021 alirejea serikalini akiwa mwanachama wa ACT-Wazalendo, na sasa ameanza tena safari yake katika nafasi hiyo baada ya kurejeshwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
0 Comments