Aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amemjibu Rais William Ruto, akisema serikali ya sasa imeendelea kumtaja na kumlaumu badala ya kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi.

Akizungumza Jumanne katika makao makuu ya Chama cha Jubilee wakati wa mkutano wa Baraza la Kitaifa la chama hicho (NEC), Kenyatta alisema alikubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita na kukabidhi madaraka kwa amani, lakini anashangazwa na matukio ya kuendelea kuhusishwa na matatizo yanayoikabili serikali ya sasa.

“Tulikubali kuwa walishinda. Miaka minne baadaye, bado ni ‘Uhuru hivi’ na ‘Uhuru vile’. Lakini mambo yanapokwenda vibaya, mnaanza kumlaumu mtu mwingine. Wakenya wana akili, wanajua ukweli,” alisema Kenyatta.

Kauli hiyo imejiri huku mvutano wa kisiasa kati ya Kenyatta na Ruto ukiendelea kujitokeza hadharani, kila upande ukieleza mtazamo wake kuhusu uongozi na hali ya nchi.

Kenyatta pia alihoji kwa nini baadhi ya viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza wamekuwa wakimtaja kama “Sponsor” yaani ''Mfadhili' 'kila anapotoa maoni yake kuhusu masuala ya kitaifa, akisisitiza kuwa demokrasia inawaruhusu viongozi kueleza misimamo yao bila kulengwa au kushambuliwa kisiasa