Mazungumzo kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na wajumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff na Jared Kushner, yalihitimishwa katika ikulu ya Kremlin baada ya mkutano wa saa tatu na dakika 10 uliolenga juhudi za kumaliza vita nchini Ukraine.

Mshauri wa Rais wa Urusi, Yuri Ushakov, alielezea mazungumzo hayo kuwa "yenye tija, ya kujenga, mazuri kabisa na yaliyojikita katika msingi wa kuaminiana," akisema kuwa hali ya mambo nchini Ukraine pamoja na masuala mengine kati ya Moscow na Washington yalijadiliwa.

Mwanzoni mwa mkutano huo, Putin alisema kuwa mawasiliano na mazungumzo na Marekani "huwa na tija kila mara," na kusifu juhudi za Trump za kutafuta suluhu ya kumaliza vita.

Wakati huo huo, Witkoff alifikisha salamu kutoka kwa Rais wa Marekani na kumshukuru Putin kwa hatua alizochukua kuhakikisha usalama wa ujumbe huo.

Putin pia aliamuru vikosi vya Urusi kutoshambulia Kyiv kwa muda wa siku tatu, kuanzia saa sita usiku wa Jumamosi, huku wajumbe hao wawili wa Marekani wakijiandaa kusafiri kwenda mji mkuu wa Ukraine.

Wakati huohuo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitangaza kuwa nchi yake iko tayari kujiepusha na mashambulizi dhidi ya Moscow hadi mwisho wa siku ya Jumatatu, akitoa wito kwa Urusi kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya Kyiv.

Alisema: "Kuanzia sasa hadi mwisho wa Jumamosi, pamoja na Jumapili na Jumatatu, Ukraine iko tayari kujiepusha na kushambulia Moscow kwa makombora, na tunatarajia Urusi ifanye vivyo hivyo kwa Kyiv."

Moscow haijatangaza kukubaliana na usitishaji wa mapigano wa siku tatu ambao ni mpana zaidi kuliko ule wa awali.

Zelensky aliongeza kuwa alizungumza na wajumbe hao wawili wa Marekani, ambao alisema "tayari wameanza ushirikiano na upande wa Urusi," akithibitisha kuwa Kyiv iko tayari kwa "mazungumzo mazito" pindi ujumbe wa Marekani utakapowasili katika mji mkuu wa Ukraine siku ya Jumapili.