Zanzibar, Septemba 20, 2026 – Wanariadha kutoka Kenya wametawala mbio za kilomita 21 za Yas Zanzibar International Marathon 2026, huku Watanzania wakifanya vizuri katika mbio za kilomita 10, katika msimu wa sita wa mashindano hayo yaliyofanyika Viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Katika mbio za kilomita 21 kwa upande wa wanaume, Wakenya Justus Nyesya, Ransisi Kamito na Simon Kelenzyo walishika nafasi tatu za juu. Kwa upande wa wanawake, Valentine Chep na Rael Mitieka kutoka Kenya walimaliza nafasi ya kwanza na ya pili, huku Mtanzania Failuna Abdi akishika nafasi ya tatu.

Katika mbio za kilomita 10 kwa wanaume, Watanzania Shedrak Damas na Boay Maganga walishika nafasi mbili za juu, huku Duncan Kipchumba wa Kenya akimaliza katika nafasi ya tatu. Kwa upande wa wanawake, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mkenya Faith Jeptum, akifuatiwa na Watanzania Anna Dolomong na Dorcas Boniface.

Akifunga mashindano hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, aliyemwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, alisema mbio hizo zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza michezo na kuitangaza Zanzibar kupitia utalii.

“Mashindano haya yana mchango mkubwa katika kukuza michezo na kuitangaza Zanzibar kama moja ya maeneo muhimu ya utalii, huku yakifungua fursa katika sekta za hoteli, usafiri, biashara na huduma mbalimbali,” alisema Mhe. Juma.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, CPA Innocent Rwetabura, alisema katika kipindi cha miaka sita, mbio hizo zimekuwa sehemu muhimu ya kuitangaza Zanzibar, kuhamasisha mtindo bora wa maisha na kuchochea uchumi wa buluu.

Rwetabura alisema Yas imeendelea kuwekeza Zanzibar, ambapo mtandao wake umeenea kwa takribani asilimia 99 ya maeneo ya Zanzibar, huku zaidi ya minara 60 mipya ikikamilishwa mwaka huu kwa kushirikiana na Serikali na UCSAF. Kupitia Yas Fiber, kampuni hiyo pia imeingia makubaliano na ZICTIA kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 300 katika miundombinu ya fiber.

Aliongeza kuwa kupitia Mixx, kampuni hiyo imeendelea kuimarisha huduma za fedha kidijitali Zanzibar, ikiwemo kurahisisha usajili na malipo ya mbio hizo kwa Watanzania. Pia imeendelea kurahisisha huduma kwa wakulima kupitia ushirikiano na ZSTC, huku ushirikiano na ZanBus ukisaidia kurahisisha malipo ya nauli kidijitali kwa wakazi wa Zanzibar.

Rwetabura alisema Mixx pia imeendelea kufanya ushirikiano mbalimbali na taasisi za Zanzibar, ikiwemo ushirikiano wa hivi karibuni na ZANGOF pamoja na ZMBF, unaolenga kupanua huduma za kidijitali kwa makundi mbalimbali, yakiwemo wakulima wa mwani.

Yas pia imeendelea na programu za kijamii Zanzibar, ikiwemo kutoa intaneti bila malipo katika shule zaidi ya 50 za Serikali, kuendesha kambi za huduma za macho na Kampeni ya Tumaini inayolenga kusaidia huduma za afya ya mama na mtoto.

Mashindano hayo yalihusisha mbio za kilomita 21, 10 na 5, na kuwakutanisha wanariadha kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali.