Zaidi ya watu 80, wengi wao wakiwa wanawake, hawajulikani walipo kufuatia matukio mawili tofauti ya utekaji nyara yaliyotokea mwishoni mwa wiki kaskazini mwa Nigeria.

Makundi yenye silaha yalivamia jamii za wakulima katika majimbo ya Niger na Zamfara.

Takriban wakulima 47 walitekwa nyara katika Jimbo la Niger siku ya Jumamosi walipokuwa wakivuna karanga, kwa mujibu wa vyanzo vya eneo hilo.

Siku iliyofuata, wanawake wapatao 40 waliripotiwa kutekwa katika Jimbo jirani la Zamfara.

Wakazi wa Zamfara walisema pia nyumba kadhaa zilichomwa moto wakati wa shambulio hilo na kuonya kwamba huenda idadi ya waliopotea ni kubwa zaidi.

Makundi wahalifu yenye silaha yamekuwa yakifanya mara kwa mara utekaji nyara na mashambulizi dhidi ya vijiji kaskazini mwa Nigeria, mara nyingi yakidai fidia ili kuwaachilia wale wanaowateka.