Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha madai kwamba ameipa Iran ahadi ya kulegezewa vikwazo na kuachiliwa kwa fedha zilizozuiliwa nje ya nchi ili ikubali kufanya maridhiano kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Kauli hiyo inafuatia ripoti ya Axios iliyodai, ikinukuu maafisa wa Marekani, kwamba Trump alikuwa tayari kulegeza baadhi ya vikwazo dhidi ya Iran kwa masharti kwamba Iran ichukue hatua madhubuti kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Akizungumza kupitia mtandao wake wa Truth Social Jumatatu jioni, Trump alisema hajatoa ahadi yoyote kwa Iran na akaitaja ripoti hiyo kuwa ya uongo.

Aidha, aliishutumu Axios kwa kuchapisha kile alichokiita habari za kutunga zinazochochewa na chuki dhidi yake.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amesema Tehran imewasilisha mapendekezo kupitia wapatanishi wa Qatar yatakayowasilishwa kwa Marekani.

Araqchi amesema anatarajia jibu la mwisho kutoka Marekani kupitia Doha siku ya Jumanne, huku juhudi za kidiplomasia za kumaliza mzozo huo zikiendelea.

Amesema pia kwamba Iran imeifahamisha Marekani na jumuiya ya kimataifa kuhusu masharti yaliyowekwa na Kiongozi Mkuu wa Iran kwa ajili ya kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, lakini hakutoa maelezo zaidi.

Araqchi ameongeza kuwa ikiwa Marekani ina nia ya kufikia makubaliano au suluhisho la amani, Iran tayari imewasilisha pendekezo lake.