AC Milan inaongoza mbio za kumsajili Endrick kwa mkopo kutoka Real Madrid mwezi Januari. Mabingwa hao wa Italia wanaamini wana nafasi nzuri ya kumpata mshambuliaji huyo wa Brazil ikiwa ataendelea kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha miamba hao wa La Liga. (La Gazzetta dello Sport)
Arsenal imeijiunga na kinyang'anyiro cha kuwania saini ya nyota chipukizi wa Mexico, Gilberto Mora. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 17, anayeichezea Club Tijuana, ana kipengele cha kuondoka chenye thamani ya pauni milioni 21.2. Hata hivyo, Washika Bunduki wanakabiliwa na ushindani kutoka Real Madrid, Barcelona, Liverpool, Borussia Dortmund na Benfica, ambazo pia zinamfuatilia kwa karibu. (El Porvenir)
Nottingham Forest inajiandaa kwa ofa zinazoweza kuwasili kwa Murillo wakati wa dirisha la Januari. Beki huyo wa kati wa Brazil mwenye umri wa miaka 24 anawindwa na Manchester United, Liverpool na Chelsea, ambazo zinaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo yake. (Teamtalk).
Bayern Munich imeonyesha nia ya kumbakisha Harry Kane kwa muda mrefu zaidi Allianz Arena. Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Christoph Freund, amesema mazungumzo ya kuongeza mkataba wa nahodha huyo wa England yanaendelea vizuri na klabu ina dhamira kubwa ya kufikia makubaliano mapya. (ESPN)
Paris Saint-Germain imeelekeza macho yake kwa Pablo Barrios, Atletico Madrid. Mabingwa hao wa Ufaransa wanaripotiwa kuwa tayari kutoa takribani euro milioni 70 ili kumnasa kiungo huyo wa Hispania mwenye umri wa miaka 23 katika dirisha lijalo la usajili. (Fichajes)
Tottenham Hotspur imeongeza juhudi za kumsaka Vangelis Pavlidis. Mshambuliaji huyo wa Benfica na timu ya taifa ya Ugiriki amejumuishwa kwenye orodha ya Spurs wanapojiandaa kuimarisha safu yao ya ushambuliaji mwezi Januari. (CaughtOffside).
Bayern Munich pia imejiunga na mbio za kumwania Luka Vuskovic. Beki huyo chipukizi wa Croatia mwenye umri wa miaka 19, anayehusishwa na Brighton, anatambuliwa kama moja ya vipaji vinavyochipukia kwa kasi Ulaya, huku Chelsea na Barcelona nazo zikiendelea kumfuatilia. (Teamtalk)
Kiungo mshambuliaji wa Barcelona Dani Olmo ameibuka kwenye rada za Bayern Munich, ambayo inaendelea kutathmini chaguzi za kuimarisha kikosi chake katika siku zijazo. (beIN Sports)
Manchester United huenda ikalazimika kuingia sokoni katika dirisha la usajili la Januari kuimarisha kikosi chake, huku changamoto katika nafasi ya beki wa kushoto na ukosefu wa ubora wa kumalizia nafasi za mabao vikiongeza shinikizo la kusajili wachezaji wapya. (The Sun)



0 Comments