Rais wa Marekani Donald Trump kwa mara nyingine ameelezea kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Kamati ya Nobel kutomtunuku Tuzo ya Amani ya Nobel, akielezea uteuzi wa mwaka huu kuwa "aibu na fedheha".

Kamati hiyo ilimtangaza jaji wa zamani wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Navi Pillay, kuwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel siku ya Ijumaa. Hata hivyo, saa chache baada ya tangazo hilo, Trump aliwaambia wafuasi wake katika mkutano wa hadhara kwamba hajawahi kumsikia mshindi huyo.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika mjini Syracuse, New York, Trump alisema uamuzi huo ni doa kwa Norway na akaonya kwamba hatua hiyo haitasahaulika kirahisi.

Rais huyo amekuwa akieleza mara kwa mara kwamba anaamini anastahili kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel. Hii si mara ya kwanza kulalamikia uamuzi wa kamati hiyo, kwani mwaka 2025 pia alikosoa tuzo hiyo baada ya kutolewa kwa kiongozi wa upinzani wa Venezuela, María Corina Machado.

Mwaka jana, Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Støre, alimkumbusha Trump kwamba mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel huchaguliwa na kamati huru ya Nobel yenye makao yake nchini Norway, na sio serikali ya nchi hiyo.

Katika hotuba yake, Trump alirudia madai kwamba alisaidia kumaliza vita nane na alikuwa karibu kusuluhisha migogoro mingine miwili, ingawa hakutoa ushahidi wa kuthibitisha kauli hizo.

"Tuzo ya Amani ya Nobel imepoteza hadhi yake kutokana na kundi dogo la watu wenye misimamo mikali wanaopinga demokrasia na ambao, kwa mtazamo wangu, ni maadui wa ustaarabu," alisema Trump