
Familia ya mfanyabiashara maarufu nchini Zimbabwe, Wicknell Chivayo, imesema itahakikisha watoto wake wanapata urithi wa mali alizoacha, huku ikimuomba Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, kuingilia kati iwapo kutakuwa na jaribio la kwenda kinyume na matakwa ya marehemu.
Kauli hiyo imetolewa na mjomba wa Chivayo na msemaji wa familia, Herbert Chivayo, wakati Rais Mnangagwa alipofika katika makazi ya marehemu yaliyopo Gletwyn, Harare, kutoa pole kwa familia kufuatia kifo chake.
Chivayo, ambaye alikuwa mfanyabiashara anayefahamika kwa maisha ya kifahari na mahusiano yake na watu mbalimbali mashuhuri, wakiwemo wanasiasa, wasanii na viongozi wa dini, alifariki Jumatano baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria kuanguka katika eneo la Kudenga Farm, karibu na Marondera.

Alifariki pamoja na mke wake, Lucy Muteke, rubani Calvin Soda, msaidizi wa rubani Courage Mutavirwa na mlinzi Saneliswe Magagula.
Akizungumza mbele ya Rais Mnangagwa na waombolezaji wengine, Herbert amesema Chivayo aliwahi kueleza mara kadhaa kuwa angependa sehemu kubwa ya mali zake irithiwe na watoto wake iwapo angefariki.
Herbert amesema familia ya Chivayo haina nia ya kugombania mali ya marehemu, akisisitiza kuwa watoto wake ndio warithi halali wa mali alizoacha.
Ameongeza kuwa familia itahakikisha matakwa hayo yanaheshimiwa na kumuomba Rais Mnangagwa kuingilia kati endapo kutatokea mtu atakayejaribu kuichukua au kuiingilia mali ya marehemu kinyume na matakwa yake.
Msiba huo umewakutanisha viongozi wa serikali na siasa, viongozi wa dini, ndugu, marafiki pamoja na maelfu ya waombolezaji waliofika kutoa heshima zao za mwisho.
Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na mwanachama wa Kamati Kuu ya Zanu PF, Kudakwashe Tagwirei, Waziri wa Habari Soda Zhemu, Waziri wa ICT Tatenda Mavetera, kiongozi wa United Family International Church Emmanuel Makandiwa, kiongozi wa dini Walter Magaya pamoja na mshauri maalum wa Rais, Paul Tungwarara.
Maelfu ya waumini wa Johanne Masowe pia walihudhuria msiba huo.
Mke wa zamani wa Chivayo, Sonja Madzikanda, alifika kwenye msiba akiwa pamoja na watoto wao wawili, ambao wameelezwa kuwa ndio watoto pekee walioachwa na marehemu.
Waombolezaji awali walikusanyika katika makazi ya mama mzazi wa Chivayo yaliyopo Borrowdale, kabla ya kuelekea katika makazi yake ya Gletwyn ambako familia ilipokea salamu za pole.
Wakati huo huo, Herbert amesema uchunguzi wa kitaalamu kuhusu miili ya waathirika wa ajali hiyo bado unaendelea.
Amesema kutokana na hali ya miili baada ya ajali, hakutakuwa na utaratibu wa waombolezaji kuuona mwili wa Chivayo kabla ya mazishi.
Familia pia imesema Chivayo anatarajiwa kuzikwa karibu na mke wake, Lucy Muteke, ingawa eneo rasmi la mazishi bado halijatangazwa.
0 Comments