Umma utaweza kushuhudia utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa njia ya kikosi cha risasi dhidi ya aliyekuwa meja wa Jeshi la Marekani, amesema Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth.

Afisa wa Idara ya Ulinzi ya Marekani ameiambia BBC kuwa utekelezaji wa hukumu dhidi ya Nidal Hasan, ambaye aliwaua wanajeshi 13 wasio na silaha katika shambulio la Fort Hood mwaka 2009, utarushwa mubashara.

Inaaminika kuwa huu unaweza kuwa utekelezaji wa kwanza wa hukumu ya kifo unaorushwa hadharani nchini Marekani katika karibu karne moja.

Mwanasheria John Mills, ambaye hufanya kazi na wafungwa waliohukumiwa kifo, amesema uamuzi wa kurusha mubashara tukio hilo ni "wa kipekee katika enzi za kisasa" na unafanyika katika mazingira yenye maswali ya kisheria.

"Tutahakikisha watu wanaweza kushuhudia, na kwamba utekelezaji huo unakuwa wa wazi kwa umma," alisema Pete Hegseth.

"Pia watu wanapaswa kuelewa kuwa matendo ya aina hii yana madhara na adhabu kubwa."

Mapema wiki hii, Pentagon ilitangaza kuwa itamtekelezea Nidal Hasan hukumu ya kifo, utekelezaji wa kwanza wa kijeshi nchini Marekani kwa zaidi ya miaka 60.

Pete Hegseth alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha kihafidhina cha Real America's Voice kwamba Nidal Hasan "atapokea adhabu ya kifo kwa kupigwa risasi na kikosi cha wanajeshi. Ndivyo inavyopaswa kuwa."

Alipoulizwa iwapo Nidal Hasan alikuwa ametoa ombi lolote la mwisho au kuwasiliana na Rais Donald Trump, Pete Hegseth alijibu:

"Sijali. Tutakutana naye tarehe 3 Desemba."

Msemaji wa Pentagon, Sean Parnell, alisema siku ya Jumatatu kwamba Pete Hegseth alikuwa ametoa pendekezo la utekelezaji wa hukumu hiyo kwa njia ya kikosi cha risasi, na kwamba Rais Donald Trump aliidhinisha uamuzi huo