Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Deogratius John Ndejembi, ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga (Uyole) hadi Ifisi jijini Mbeya, akihoji maendeleo ya kazi hiyo licha ya mkandarasi kupata fedha zinazofikia Shilingi bilioni 40 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika eneo la Kabwe jijini Mbeya, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, Makamu wa Rais amesema Serikali inatarajia kuona kasi ya utekelezaji wa mradi ikiendana na fedha zilizotolewa, huku akieleza kuwa wananchi wameendelea kukabiliwa na changamoto za vumbi, kufungwa kwa barabara na kukwama kwa shughuli za biashara na usafiri.

Amesema mkandarasi huyo alipokea malipo ya awali ya Shilingi bilioni 20 na kuonyesha uwezo wa kupata fedha nyingine Shilingi bilioni 20 kupitia benki, hali inayofanya Serikali kutarajia maendeleo yanayoonekana katika utekelezaji wa mradi huo.

Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Rais amemwelekeza Waziri wa Ujenzi kuhakikisha barabara zilizofungwa zinafunguliwa kuanzia kesho ili kupunguza adha wanazopata wananchi, wafanyabiashara na watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Amesisitiza kuwa kipaumbele kinapaswa kuwekwa katika kipande cha barabara kinachopita katikati ya Jiji la Mbeya, hususan eneo la Mwanjelwa, kutokana na umuhimu wake katika shughuli za usafiri na biashara.

Ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulipaswa kutekelezwa kwa awamu ili kuruhusu shughuli za kiuchumi kuendelea bila kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na kazi za ujenzi.

Awali, Makamu wa Rais alipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa barabara ya Nsalaga–Ifisi wenye urefu wa kilometa 29 na gharama ya Shilingi bilioni 183.708.

Taarifa hiyo pia ilihusisha maendeleo ya miradi mingine ya miundombinu mkoani Mbeya, ikiwemo barabara ya Katumba–Lupaso iliyofikia asilimia 6.6, barabara ya Mbaka–Kibanja iliyofikia asilimia 0.3, pamoja na Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani Kasumulu/Songwe ambacho kimefikia asilimia 94.46 ya utekelezaji.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza ufanisi wa usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia watendaji na wakandarasi ili kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika ipasavyo na miradi hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia matarajio ya wananchi.

Ameeleza kuwa usimamizi huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya uwekezaji wa Serikali kwa wakati, huku changamoto zinazotokana na utekelezaji wa miradi zikipatiwa ufumbuzi wa haraka.