Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imesema kuwa raia wawili wa Bangladesh, mwanamume na mwanamke, wamehukumiwa kifo na kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kufanya kile kilichoelezwa kama "vitendo vya aibu" ndani ya msikiti katika mji mtakatifu wa Makka.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA), likinukuu taarifa ya Wizara hiyo, mwanamume huyo aliyetambuliwa kwa jina la Nazrul Islam Abdul Basir na mwanamke Siti Akhtar walikabiliwa na mashtaka ya kufanya vitendo hivyo ndani ya moja ya misikiti ya Makka.

Baada ya tukio hilo, maafisa wa usalama waliwakamata wawili hao na kuwafikisha mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi yao.

Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema mahakama iliwapata na hatia na kuwahukumu adhabu ya kifo, ikizingatia uzito wa kosa hilo, mazingira ya tukio, pamoja na kile ilichokitaja kuwa ukiukwaji wa utakatifu na heshima ya msikiti.

Kwa mujibu wa maafisa wa Saudi Arabia, hukumu hiyo ilikatiwa rufaa, lakini Mahakama ya Juu ilitupilia mbali ombi hilo na kuidhinisha uamuzi wa mahakama ya awali.

Baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria, amri ya kifalme ilitolewa kuruhusu utekelezaji wa hukumu, ambao ulitekelezwa Jumatano, Oktoba 14.