
MWANZA; Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, amewataka watumishi wa umma kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi, huku wakitoa huduma bora kwa wananchi kwa uadilifu, bila ubaguzi.
Makonda ameyasema hayo leo jijini Mwanza katika uzinduzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.
Amesisitiza kuwa wananchi wanaolipa kodi wanastahili kuhudumiwa kwa heshima, ukarimu na unyenyekevu, akiwataka watumishi kutokata tamaa wanapopangiwa majukumu katika maeneo tofauti, kwani hali hiyo huwapa uzoefu na kuwaandaa kwa majukumu makubwa zaidi.
Amesema ubora wa huduma za umma haupimwi kwa uzuri wa majengo pekee, bali pia kwa tabia, weledi na uwajibikaji wa watumishi.
Ameonya kuwa wananchi hawapaswi kuzungushwa kutoka idara moja kwenda nyingine au kuambiwa warudi siku nyingine bila sababu za msingi, akieleza kuwa huduma duni hudhoofisha imani ya wananchi kwa serikali.
Katika hatua nyingine, Makonda ametangaza zawadi ya gari aina ya IST kwa Jenitha Byagalama, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ukerewe, akitambua utumishi wake wa muda mrefu, uaminifu na kujituma. Amesema Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai, atakabidhi gari hilo wiki ijayo.
Akitoa taarifa ya mradi, Mhandisi wa halmashauri hiyo, Lufundya Katemi, amesema serikali imetoa Sh bilioni tatu, sawa na asilimia 91.05 ya gharama zote za ujenzi katika kipindi cha fedha 2022/2023 hadi 2025/2026.
Amesema jengo hilo lina ofisi 49, kumbi mbili za mikutano, divisheni tisa na vitengo 11, na lilianza kutumika rasmi Mei 2026. Kwa sasa, Shilingi milioni 300 zinahitajika kununua samani.
0 Comments