Mahema ya Wapalestina waliokoseshwa makazi yanaonekana katika mji wa Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Kufuatia shambulizi la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023, Israel ilianzisha operesheni kubwa ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza, hatua iliyosababisha zaidi ya watu milioni moja kuhama makazi yao na vifo vya makumi ya maelfu ya watu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, takribani watu 74,200 wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu kuanza kwa vita hivyo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) inasema mahitaji ya kibinadamu katika Gaza bado ni makubwa sana, huku watu wengi wakikabiliwa na uhaba wa maji safi, chakula na dawa.

Umoja wa Mataifa pia unakadiria kuwa karibu asilimia 80 ya majengo yote katika Gaza yameharibiwa au kuathiriwa na vita kati ya Israel na Hamas.

Zaidi ya watu milioni 1.9, sawa na karibu asilimia 90 ya wakazi wa Gaza, wamekoseshwa makazi, wengi wao wakihama mara kadhaa. Kati yao, takribani milioni 1.2 kwa sasa wanaishi katika mahema au makazi ya muda.

Mwaka jana, jumuiya kubwa zaidi duniani ya wataalamu wa tafiti za mauaji ya kimbari ilitangaza kuwa Israel ilikuwa ikifanya mauaji ya kimbari huko Gaza. Israel imekuwa ikikanusha madai hayo mara kwa mara, ikisema operesheni zake za kijeshi ni sehemu ya haki yake ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Hamas.

Ingawa makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza kutekelezwa Oktoba mwaka jana, mashambulizi ya anga ya Israel na operesheni katika maeneo yenye wakazi wengi yameripotiwa kuendelea katika baadhi ya sehemu za Gaza.