Cristiano Ronaldo amefunga mabao 146 akiichezea Ureno katika mechi 234.

Nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo, amesema yuko tayari kuwajibika kwa kuondoka kambini mwa timu ya taifa, lakini amemtuhumu kocha mkuu Jorge Jesus kwa kuvunja ahadi aliyompa mara mbili.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 41 aliondoka kambini wiki iliyopita baada ya kutochezeshwa katika mchezo dhidi ya Norway na baadaye kufahamishwa kuwa hangeanza katika mechi dhidi ya Denmark kwenye Nations League.

Katika taarifa ndefu aliyotoa, Ronaldo alikiri kuwa hatua yake ilikuwa na matokeo na kusema yuko tayari kukubali adhabu yoyote itakayoamuliwa na Shirikisho la Soka la Ureno.

"Shirikisho la Soka la Ureno lazima litathmini matokeo ya matendo yangu na kuniadhibu. Ninaamini adhabu hiyo haipaswi kupunguzwa," alisema.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Al-Nassr alisema alihisi kusalitiwa baada ya kocha Jesus kushindwa kutimiza ahadi ya kumchezesha dhidi ya Norway, jambo alilolitaja kuwa "uvunjifu mkubwa wa imani".

Licha ya sakata hilo, Ronaldo amesisitiza kuwa hana mpango wa kustaafu soka la kimataifa. Mfungaji huyo wa mabao 146 katika mechi 234 za Ureno amesema bado anatamani kuendelea kuitumikia nchi yake ikiwa ataendelea kuwa fiti na kufanya vizuri klabuni.

"Baada ya kipindi changu cha kusimamishwa kumalizika, nitakuwa tayari, kama nilivyokuwa siku zote, kushindana na kushinda na timu yetu ya taifa."

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Jesus kusisitiza kuwa hakuna mgogoro kati yake na Ronaldo na kwamba mlango bado uko wazi kwa nyota huyo kuendelea kuichezea Ureno.