Rajapaksa alikamatwa siku mbili baada ya kurejea Sri Lanka kutoka Singapore

Mke wa rais wa zamani wa Sri Lanka, Shiranthi Rajapaksa, amekamatwa kwa madai kwamba shirika la kutoa misaada linahusishwa na michango iliyochangishwa vibaya kwa ajili ya hospitali ya watoto.

Mamlaka ya kupambana na ufisadi ilimkamata mke huyo wa Rais wa zamani Mahinda Rajapaksa mwenye umri wa miaka 73 nyumbani kwao Colombo siku ya Jumatano.

Wanamhoji kuhusu rupia milioni 10 ($30,300; £22,800) za michango iliyokusanywa na shirika la hisani la Siriliya Saviya, zilizokusudiwa kutumika kwenye skana maalum kwa ajili ya Hospitali ya Watoto ya Lady Ridgeway ya Colombo.

Lakini maafisa wanasema skana kama hiyo tayari ilikuwa imetolewa na serikali ya China.

Shiranthi Rajapaksa amekanusha kosa lolote na anasema pesa hizo hazijachukuliwa.

Alirudi Sri Lanka Jumatatu kutoka Singapore, ambapo alikuwa akipokea matibabu. Alikuwa amewasilisha ombi mahakamani kujaribu kuzuia kukamatwa kwake, lakini kikao cha mahakama kimepangwa kufanyika tarehe 12 Oktoba kusikiliza kesi yake.

Msemaji wa Rais wa zamani Mahinda Rajapaksa, Manoj Gamage, amesema pesa hizo ziko salama katika akaunti za Siriliya na kwamba hakuna ulaghai wowote uliotokea.

Mahinda Rajapaksa alihudumu kama rais wa Sri Lanka kuanzia 2005 hadi 2015. Alisifiwa na wengi kama shujaa kwa kukomesha karibu miongo mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati waasi wa Tamil Tiger walipoangamizwa mwaka wa 2009, wakati wa muhula wake wa kwanza kama rais.