Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP), imeendelea kuimarisha ushiriki wa jamii katika kukabiliana na changamoto za VVU na UKIMWI kupitia mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo viongozi na wadau wa afya katika kutambua changamoto na kutafuta suluhisho zinazozingatia mazingira halisi ya jamii.


Mafunzo hayo yamefanyika Mkoani Morogoro na ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa miaka miwili unaofadhiliwa na Global Fund katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Geita, Dodoma na Singida.

Kupitia mafunzo hayo ya Adaptive Leadership, washiriki wamejengewa uwezo wa kuchambua changamoto za afya kulingana na mazingira ya jamii, kushirikisha wadau mbalimbali na kuandaa suluhisho endelevu, hususan katika kukabiliana na VVU na magonjwa ya ngono.

Mwanaharuna Ramadhani Saidi, muelimishaji rika kutoka Taasisi ya TAYOA mkoani Morogoro, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa kwa kina mazingira yanayoweza kuchangia maambukizi ya VVU miongoni mwa vijana, ikiwemo maeneo ya starehe, matumizi ya dawa za kulevya na maeneo ya uchimbaji wa madini.

Amesema changamoto ya maambukizi ya VVU haiwezi kuhusishwa na wingi wa watu pekee katika eneo fulani, bali inapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia sababu mbalimbali za kijamii na kitabia zinazowazunguka vijana.

Kwa upande wake, Hezron Yuda, Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Wilaya ya Chato mkoani Geita, amesema mafunzo hayo yamempa uelewa zaidi kuhusu umuhimu wa kuishirikisha jamii katika kutambua changamoto za afya na kushiriki katika kutafuta suluhisho.

Amesema wataalamu wanapaswa kutambua kuwa jamii yenyewe ina maarifa muhimu kuhusu changamoto zinazowakabili, hivyo ushirikishwaji wake unaweza kusaidia kupata suluhisho linaloendana na mazingira na mahitaji halisi ya wananchi.

Naye Ayubu Bwanamadi, Kiongozi wa Dini ya Kiislamu na Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa Kiislamu mkoani Geita, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa kuwa uongozi si suala la kuwa na nafasi au mamlaka pekee, bali ni wajibu wa kutumia nafasi hiyo kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Amesema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kuwafikia vijana, kuwaelimisha kuhusu afya, maadili na namna ya kujikinga dhidi ya VVU na magonjwa ya ngono.

Washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika Dodoma wameitaka Serikali na wadau wa afya kuendelea kuwekeza katika elimu kwa vijana, kuimarisha ushiriki wa jamii na kuhakikisha afua za kukabiliana na VVU zinazingatia mazingira halisi ya wananchi.

Wamesema ushiriki wa jamii na uongozi unaozingatia changamoto zilizopo katika mazingira husika ni muhimu katika kuhakikisha jitihada za kuzuia maambukizi ya VVU na magonjwa ya ngono zinakuwa na matokeo endelevu.