
MOROGORO. Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro, unaogharimu Sh bilioni 336, umefikia asilimia 70 ya utekelezaji.
Mhandisi Kundo aliyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wa kimkakati, unaotekelezwa katika eneo la Ngerengere mkoani humo.
Alisema kukamilika kwa bwawa hilo kutasaidia kumaliza changamoto ya uhaba wa maji katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2050.

“Bwawa hili ni suluhisho la kudumu. Litahifadhi lita bilioni 190 za maji na kuhakikisha mitambo yetu ya Ruvu Juu na Ruvu Chini inapata maji muda wote, hata wakati wa kiangazi, ambapo zaidi ya wananchi milioni saba watanufaika,” alisema Mhandisi Kundo.
Alifafanua kuwa kati ya maji yatakayozalishwa kwa siku, lita milioni 600 zitaelekezwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), huku lita milioni 400 zikitumika katika mashamba ya sukari ya Mkulazi.

Alisema zaidi ya lita milioni 900 zitaendelea kutiririka mtoni kwa ajili ya kulinda ikolojia na mazingira katika ukanda huo.
Aidha, Mhandisi Kundo alisema bwawa hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuwa litazalisha megawati 20 za umeme zitakazoingizwa katika Gridi ya Taifa kupitia njia ya umeme yenye urefu wa zaidi ya kilometa 100 kutoka Kidunda hadi Chalinze.
Alisema mradi huo pia utafungua fursa katika sekta za kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na utalii, hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka bwawa hilo.
“Mradi huu ulisuasua tangu mwaka 1961, lakini kutokana na dhamira ya Rais Samia, leo tunaona ujenzi ukiendelea usiku na mchana. Hii ndiyo maana ya uchumi wa maji tuliouandaa kwenye Dira ya 2050,” alisema.

Mhandisi Kundo aliwataka wakandarasi wanaotekeleza mradi huo, unaosimamiwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu, kuhakikisha wanazingatia ubora wa kazi na kuukamilisha kwa wakati kama ilivyopangwa.
Alisema Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha mradi huo unakamilika, hivyo wakandarasi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viwango na muda uliowekwa.
0 Comments