GEITA: WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ameitaka Wizara ya Madini kuendeleza usimamizi thabiti wa sekta ya madini ili kuongeza tija kuelekea dira ya maendeleo ya taifa 2050.

Dk Mwigulu ametoa maelekezo hayo wakati akifunga Maonyesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika viwanja vya Dk Samia Suluhu Hassani Manispaa ya Geita.

Amesema kwa kurejea kauli mbiu ya maonyesho hayo, Madini ni Uatajiri, Tuwajibike kwa Pamoja, kufikia Dira ya Taifa 2050 kila mmoja anao wajibu wa kusimamia kwa ufasaha sekta ya madini.

“Kauli mbiu hii imekuja kwa wakati muafaka, kwa kuzingatia utajiri mkubwa wa madini, tuliojaariwa kama taifa”, amesema Dk Mwigulu.

Amesema tayari serikali imeshaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 inayotoa mwelekeo wa kujenga uchumi shindani, jumuishi, unaotegemea maarifa, ubunifu na matumizi ya teknolojia.

Amesema kwa kutambua kuwa sekta ya madini ni nguzo muhimu ya uchumi wa taifa serikali imepitisha mabadiliko ya sheria inayoagiza asilimia 10 ya mapato ya madini iende katika utafiti.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mpaka sasa Tanzania imefikia asilimia 16 ya utafiti wa madini huku kupitia sheria mpya usimamizi unaendelea kuimarishwa kupanua uwigo zaidi.

Amesema elimu kwa wachimbaji wadogo inaendelea kutolewa kuhakikisha kwamba wanaendana na matumizi ya sayansi na teknolojia na kuachana na dhana potofu kutumia imani za kishirikina.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti amesema kuwa Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yameendelea kutumika kama nyenzo ya kupanua uwigo wa matumizi ya teknolojia migodini.

“Tunapaswa kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazotambua maeneo yenye madini, kuongeza ufanisi na uchimbaji na uchenjuaji ili kupunguz aupotevu wa madini”, amesema.

Amesema pia ipo haja ya kuongeza uwekezaji katika uchakataji wa madini nchini ili taifa lisibakie mzalishaji wa madini pekee bali mhimili wa mnyororo wa thamani migodini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML), Ashraf Suryaningrat amesema kampuni hiyo inayo dhamira ya dhati ya kushirikiana na serikali kukuza sekta ya madini.

Amesema kwa kurejea dira ya Taifa ya 2050, GGML wamejizajititi kuzalisha siyo tu raslimali madini bali pia kuzalisha raslimali watu wenye ujuzi, maarifa na uwezo kuelekea uchimbaji wa kisasa.