Luteni Jenerali Shadrack Sibiya amekanusha mashtaka yote yanayomkabili.

Wakili anayemwakilisha Luteni Jenerali Shadrack Sibiya aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu wakati wa kikao cha kinidhamu Jumatatu, msemaji wa polisi amesema.

Mashtaka hayo yanahusiana na madai kwamba alimshawishi na kumwandaa msichana mwenye umri wa miaka 16 kwa ajili ya unyanyasaji wa kingono, na kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 18. Pia anakabiliwa na shtaka la usafirishaji haramu wa binadamu.

Sibiya amekanusha mashtaka yote. Lakini amekiri kufanya ngono na mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 18, lakini anasema walikubaliana kufanya hivyo.

Amekuwa kizuizini tangu alipokamatwa wiki tatu zilizopita, baada ya ombi lake la dhamana kukataliwa.

Msemaji wa polisi, Athlenda Mathe, alisema katika chapisho kwenye mtandao wa X kwamba kuondoka kwa Sibiya katika jeshi la polisi kunachukuliwa kuwa kufukuzwa kwa aibu.

Kesi hiyo imeibuka wakati jeshi la polisi likichunguzwa katika tume kubwa ya uchunguzi wa umma kuhusu madai ya ufisadi na kushirikiana na wahalifu.

Uchunguzi huo, unaojulikana kama Tume ya Madlanga, ulianza Septemba 2025 na umesikiliza madai kwamba Sibiya alipokea zawadi ya swala 20 kutoka kwa mtu anayedaiwa kuwa kinara wa uhalifu, kama malipo ya kumpatia mkataba wa polisi.